Dk. Samia anavyosafiri na Awamu ya Sita kuhuisha zama za ‘Tanzania ya Viwanda’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:59 PM Jan 03 2025
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akitangazia wakazi wa mkoa Morogoro serikali inavyojipanga kurejesha hadhi yake kuwa Mkoa wa wa Viwanda, kama ilivyokuwa awali.
Picha:Mtandao
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akitangazia wakazi wa mkoa Morogoro serikali inavyojipanga kurejesha hadhi yake kuwa Mkoa wa wa Viwanda, kama ilivyokuwa awali.

JANA gazeti hili lilikuwa na uchambuzi unaohusu hatua na nyendo za Serikali ya Awamu ya Sita kimaendeleo, ikiangaziwa mwenendo, utekelezaji, uwekezaji katika afya, pia dira yake.

Maudhui yake mahsusi, yanaangazia afya ya mwanamke na mtoto, ambayo ndiyo ajenda muhimu nchini na duniani.

Lakini katika sura ya pili, kuna ngazi ya maendeleo, ambayo nyenzo mojawapo ni kupitia uchumi, ambao sekta ya viwanda kitaifa ni eneo muhimu sana.

Miaka mitatu iliyopita, Dk. Philip Mpango, Makamu wa Rais katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akaitoIea ufafanuzi, akiwa na maelezo kwa niaba ya mkuu wa nchi akisema:

“Sekta ya viwanda ndio chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi mbalimbali na mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuongeza thamani ya malighafi tulizo nazo, kutoa ajira kwa wananchi,” 

Dk. Mpango akaendelea kutaja mengine: “…na kuongeza mapato ya serikali, pamoja na fedha za kigeni na kuongeza kuboresha sayansi na teknolojia.” 

Ilikuwa katika tukio lililofanyika Oktoba mwaka 2021 ikiwa ni hafla ya kutoa Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora wa Viwanda nchini iliyoandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara jijini Dar es Salaam.

Akasisitiza msimamo wa Sekta ya Viwanda katika zama Awamu ya Sita ya Rais Dk. Samia, ina jukumu la kuhakikisha nchi inapenya katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na lile la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),

Dk. Mpango akasisitiza haja ya kuhakikisha kunakuwapo uuzaji bidhaa katika soko la EAC unaongezeka kufika asilimia 15 kwa hatua ya wakati huo, lengo ni asilimia 30 wa soko lote.  Ilikofika ilikuwa asilimia saba. 

Akataka namna mojawapo akiitaja ni: “Kupenda kununua bidhaa za nje kuna madhara makubwa kwenye ukuaji wa viwanda vyetu, kwa kuwa inasaidia viwanda vya nje viendelee kukua pia kuhamisha ajira kutoka nchini kwetu kwenda nchi za wenzetu”

KUTOKA KWA RAIS 

NI wiki hii, katika kuukaribisha Rais Dk. Samia akatimiza malengo yake kwa vitendo, alipofahamisha sehemu ya mavuno ya azma yake, akisema viwanda vipya vikubwa 15 viko ‘jikoni’ vinajengwa.

Hiyo inatamkwa na Rais, huku katika chombo cha habari na Ofisa wa Tume ya Uwekezaji (TIC), kwamba mwaka jana juhudi za Rais Dk. Samia imeweka rekodi, kwani kumesajiliwa miradi wastani 900, ikivuka rekodi kubwa ya awali ya miradi 500.

Mnamo Agosti mwaka huu, Rais Dk. Samia, akawaagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo kuanza mchakato wa mabadiliko ya sera ili viwanda vya sukari vya ndani viwe na uwezo wa kuzalisha sukari ya viwandani na malighafi ya kuzalisha nishati safi ya kupikia na matumizi mengine. 

Hapo akafafanua ni hatua ya kupunguza pengo la upatikanaji sukari nchini, kwani mahitaji ya sukari nchini ni tani 650,000 huku viwandani ni tani 250,000, akisistiza kuendelea kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi ni matumizi mabaya ya fedha za kigeni.

Pia, ndani ya mtazamo huo, akawa na ufafanuzi kwamba, dhamira ya serikali yake ni kulinda viwanda, pia kuwalinda walaji.

Hapo alikuwa anazuru mkoani Morogoro katika uzinduzi wa upanuzi wa mashamba ya sukari na umwagiliaji, ili kuwa na kilimo cha uzalishaji wa kisasa.

“Tunalenga kufikisha sukari tunayozalisha Jamhuri ya Watu wa Congo (DRC) na nchi nyingine kwa kuzidi kuboresha miundombino ya usafiri na uzalishaji ili kupanua wigo wa masoko ndani na nje ya nchi kwa kuongeza tija,” akasema Rais Dk. Samia.

Kiwanda hicho cha sukari kimefunga mitambo ya kisasa 47 inayofanya kazi kati ya 112 inayopaswa kujengwa, itakayoongeza uchakataji wa miwa kutoka tani 100 hadi 180 kwa saa.

Hapo kukafafanuliwa matarajio yake kwamba ni kufikia mwaka 2027 itachakata tani 230 za miwa kwa saa, ikiendana na kutolewa ajira zinazofika 10,000.

MIPANGO VIWANDA ILIVYO 

Hatua za kuibua na kendeleza viwanda nchini, inatajwa kuwamo katika muhtasari wa Wizara ya Viwanda na Biashara, inatekeleza majukumu yake ya kimuundo kwa kuzingatia maelekezo ya viongozi wakuu wa serikali.

Kurejea miongozo ya wizara husika na viwanda, ni maelekezo yanayotajwa kuwamo katika mipango ya kitaifa na kimataifa, kama ilivyoainishwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs 2030), vilevile Ajenda ya Afrika 2063.

Maeneo mengine nchini yanatajwa kuwa ni: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2020; na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26.

Pia, katika kuchochea kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini, wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kufanya mapitio ya Sera, Mikakati na Sheria za kisekta.

Hapo dhamira ni kuziwezesha kuendana na mahitaji ya sasa. Anazitaja sera hizo ni pamoja na sera za taifa za: Uhamasishaji Uwekezaji (1996); Maendeleo Endelevu ya Viwanda (SIDP, 1996 - 2020); Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (2003); Masoko ya Mazao ya Kilimo (2003); na Sera ya Taifa ya Biashara (2003). 

Msukumo huo unaoibua viwanda nchini, inatajwa ni sehemu ya kazi za Wizara ya Viwanda na Biashara, ikienda sambamba na sheria, pia mikakati ya kisekta, ikiwamo inayoendeleza Sekta ya Ngozi na Bidhaa za Ngozi; Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Pamba, Nguo hadi Mavazi (C2C); Mkakati wa Kuendeleza Zao la Alizeti; Sheria ya Kujilinda dhidi ya Athari za Kibiashara; sheria za uwekezaji, pia ushindani ya mwaka 2003.

Viwanda, ndio suala linalotamba hivi sasa katika majukwaa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani na nje ya Tanzania.