BARAZA la Mchele Tanzania (RCT), limewashauri wakulima wa zao la mpunga kujikita katika matumizi ya mbegu za kisasa zinazoendana na matumizi sahihi ya mbolea na udongo uliopimwa ili kujua mahitaji na virutibisho vinavyohitajika.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hilo, Geofrey Rwiza, alisema hayo wakati wa kuhitimishwa kwa mradi wa kujenga uwezo kubadilishana uzoefu masuala ya uongezaji wa thamani katika zao la mpunga ulianza kutekelezwa mwaka 2020 na kufikia tamati Desemba 2024.
Alisema matumizi hayo yanachangia kupatikana kwa ubora wa zao hilo na kupata kiwango bora cha mchele wa daraja la kwanza na kuwanufaisha wakulima katika soko la ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema kwa sasa matumizi ya mbegu bora yasiyoendana na aina ya mbolea inayopaswa kutumika yamechangia zao la mpunga kushinmdwa kupatikana kwa wingi mchele wa daraja la kwanza nchini.
“Hivi sasa mbegu nyingi zinazoendelezwa zinaendana vizuri na matumizi ya mbolea ikiwamo ya Natrojeni hivyo wakulima lazima wangalie hilo pamoja na kuangalia soko,” alisema Rwiza.
Alisema kwa sasa Baraza hilo linawahamasisha wakulima wa zao hilo kuzingatia matumizi ya mbegu za kisasa na kuambatana na matumizi sahihi ya mbolea na kuvuna kwa wakati.
“Teknolojia hizo zitasaidia kurudisha hali ya kupata viwango vya mchele utakaopangwa kimadaraja na hasa uwingi wa upatikanaji wa mchele wa daraja la kwanza nchini,” alisema Rwiza.
Kuhusu mbegu za kienyeji ambazo hazitumii mbolea, alisema kuwa mchele wake ukipangwa kwenye madaraja unapatikana kuwa ni mzuri kwa sababu ya kutotumia hizo mbolea.
“Nashauri matumizi sahihi ya mbolea na udongo yawe umepimwa ili kujua unahitaji virutubisho gani na si kuweka mbolea tu, pia kuweka kwa wakati unaopaswa ili maji yanapoingia shambani kusiwe na kupishana lengo kuwe na kalenda ya uwekaji mbolea na uvunaji kwa wakati,” alisisitiza Rwiza.
Mmoja wa wakulima wa Kijiji cha Wami Dakawa, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Nyaguso Lemwai, alisema amenufaika na mafunzo ya kilimo endelevu cha mpunga chini ya mradi huo ambao ulilenga namna bora ya matumizi ya mbegu bora za mpunga.
Alisema pia namna ya kuendesha kilimo cha kitalu mkeka kwa maana ya kutumia mbegu chache katika eneo kubwa na matumizi sahihi ya mbolea na maji ikiwa na matumizi ya zana bora za kilimo hicho na kuwezesha kuongeza kiwango cha uzalishaji na kipato kukua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED