Jussa, wanachama ACT wasema Othman anatosha urais Zanzibar

By Rahma Suleiman ,, Joyce Lameck , Nipashe
Published at 12:54 PM Jan 03 2025
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman akiwa na Mjumbe wa Baraza Kuu wa chama hicho, Ismail Jussa Ladhu.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman akiwa na Mjumbe wa Baraza Kuu wa chama hicho, Ismail Jussa Ladhu.

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, kutangaza nia ya kugombea urais wa Zanzibar, baadhi ya viongozi wa chama hicho wamesema "anatosha".

Waliosema Othman ana sifa za kupeperusha bendera ya ACT-Wazalendo kwenye Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, wametaja sifa ya uzoefu na uadilifu kama nyenzo itakayokipa chama hicho ushindi.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alitangaza nia ya kugombea urais visiwani humo juzi alipozungumza na wahariri mjini Unguja katika salamu zake za Mwaka Mpya 2025.

Katibu Mkuu wa Baraza Kivuli la ACT-Wazalendo, Seif Hamad Suleiman, alisema Othman ni mtu sahihi kwa wakati sahihi kwa sababu historia yake kwenye utumishi wa umma ni nzuri.

Alisema Othman ametumikia Serikali ya Zanzibar kwa zaidi ya miaka 30 na kuteuliwa nyadhifa mbalimbali, ikiwamo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hajawahi kuwa na kashfa.

Alisema Othman ana uwezo mkubwa kiutendaji, hivyo anaweza kuivusha Zanzibar kuwa na maendeleo zaidi.

Mjumbe wa Baraza Kuu wa chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, alisema Othman ni mtu sahihi na chama kinamwamini kwa sababu hana tabia ya kupindisha maneno na kwamba ni mtu mwenye msimamo imara.

Alisema Othman ana sifa zote zinazohitajika na ana vigezo vya kuwa mgombea urais wa Zanzibar na wakati utakapofika chama kitamuunga mkono.

Katibu wa Idara ya Habari ACT-Wazalendo, Salum Bimani alimpongeza Othman kwa kutangaza nia hiyo mapema.

Alisema ana imani na kiongozi huyo kuwa anao uwezo wa kuwania nafasi hiyo kwa kuwa ni kiongozi mzuri na anastahili kupeperusha bendera ya ACT-Wazalendo Oktoba mwaka huu.

"Siamini kama kuna mtu anaweza kuchukua fomu kwa mapenzi yake ili kushindana na Othman katika viwango vyake vyote kitaifa na kimataifa, ni mgombea anayeuzika na kununulika pia, ni bidhaa nzuri na yenye soko kwa uchaguzi wa Oktoba 2025," alisema Bimani.

Mmoja wa wanachama wa chama hicho, Hassan Njani, alisema ni vizuri kiongozi kujitangaza mapema ili kuwapa wananchi nafasi katika kuamua kama atafaa katika kuongoza.

"Unapojitangaza mapema kuwania nafasi, wananchi wanapata muda mzuri wa kutafakari juu ya uadilifu wako katika maisha ya siasa, ili kukupima na kukutambua una vigezo vyote ambavyo vinafaa kuwa kiongozi hasa kwa nafasi hiyo juu ya uongozi wa serikali," alisema.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa, akizungumzia suala hilo, alisema ni haki ya kiongozi kutia nia mapema kwa kuwa inampa nafasi ya kujiandaa kwa ajili ya kuwa kiongozi mzuri.

Pia inasaidia wananchi kufanya uamuzi sahihi katika kumchagua kiongozi sahihi na mwenye kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kumtambua kama aweza kuwa kiongozi kwao.

Othman ametangaza kuwania urais wa Zanzibar akitaja kusimamia mambo 11, aliyosema yatavipaisha visiwa hivyo kimaendeleo, akiyataja yanajumuisha kujenga ustawi wa uchumi, kuwarejeshea wananchi haki ya kuwawajibisha viongozi na kujenga misingi ya utawala bora.

Pia alitangaza msimamo wa chama chake kwamba kitashiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, bila kujali hali ya kisiasa iliyopo nchini.