Yanga: Ama zao, ama zetu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:22 PM Jan 03 2025
Yanga: Ama zao, ama zetu.
Picha:Mtandao
Yanga: Ama zao, ama zetu.

WAWAKILISHI pekee wa nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wamesema mechi dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ni daraja lao la kuvuka kwenda hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya kimataifa.

Yanga pia imesema haivutii kuona timu yao inashika nafasi ya mwisho katika msimamo wa Kundi A ikiwa na pointi moja tu huku kinara akiwa ni Al Hilal ya Sudan yenye pointi tisa.

Akizungumza jijini jana, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema wamekaa na wachezaji na kukubaliana mechi ya kesho watacheza kama hakuna mchezo mwingine watakaocheza tena kwa sababu ndio utakuwa daraja la wao kwenda hatua mbele ya michuano hiyo, vinginevyo watakuwa wamejiweka katika hali mbaya.

Kamwe alisema wakati wachezaji wakihamasishana 'kufia uwanjani' katika mechi hiyo, amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwashangilia na kuwapa hamasa na kuufanya Uwanja wa Benjamin Mkapa uwe kama 'tanuri la moto' kwa wapinzani.

Alisema haipendezi kwa klabu kama Yanga ambayo msimu uliopita ilifika hatua ya robo fainali ishike mkia katika kundi kutokana na kuvuna pointi moja pekee baada ya kucheza michezo mitatu.

"Wanachama na mashabiki wa Yanga, naweza kutumia maneno mengi ili kujua  mchezo huu una umuhimu mkubwa kwetu. Ukweli ambao utaendelea kubakia na hatuwezi kuuepuka na unatuonesha kwa picha inayoumiza ni pale tunapolitazama kundi letu, haipendezi na haivutii, lakini ndiyo ukweli, kwenye kundi letu tuna pointi moja tu, ambayo tumeipata katika michezo mitatu. Ukweli huo hauishii hapo, bali tunashika nafasi ya mwisho," alisema Kamwe.

Aliongeza ukweli huo ndiyo iwe chachu kwa Wanayanga kufanya kitu kwa ajili ya timu yao, na hakuna kingine ila kujitokeza kwa ajili ya kuujaza uwanja kwa lengo la kuwatoa mchezoni TP Mazembe.

"Ukweli huu mchungu unapaswa kuwa hamasa namba moja kwa kila Mwanayanga anapoufikiria mchezo huo. Nasema ukweli mchungu kwa sababu hauhitaji propaganda wala siasa, hatukuanza vizuri michuano hii, sasa tunahitaji pointi tatu ili tuinuke, tutoke mwisho wa msimamo, sisi ni timu kubwa haiwezekani tuendelee kukaa huko," Kamwe alisema.

Kuhusu maandalizi alisema, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, ameendelea kukinoa kikosi na kuangalia wachezaji ambao anaweza kuwatumia katika mechi hiyo huku waliokuwa majeruhi wakianza kujifua pamoja na wenzao.

"Golikipa wetu Djigui Diarra, Maxi Nzengeli na Clatous Chama wameshaanza mazoezi na kikosi kwa ajili ya mchezo huo, ila Yao Kouassi bado afya yake na utimamu wa mwili haujakuwa sawa, hajaanza mazoezi, hivyo hatakuwa sehemu ya kikosi," alisema Kamwe.

Kikosi cha TP Mazembe kilitarajiwa kutua nchini jana jioni, tayari kwa ajili ya mchezo huo wa raundi ya nne, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 mjini Lubumbashi, hapo Desemba 14, mwaka jana.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walianza hatua hiyo ya makundi kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0 hapa nyumbani kutoka kwa Al Hilal na ikiwa ugenini kufungwa idadi kama hiyo na MC Alger ya Algeria.