Serikali katika mapinduzi maendeleo, kupitia ubunifu wa teknolojia za vijana

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 01:26 PM Jan 03 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, akimsikiliza mbunifu wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa COSTECH Dk. Amos Nungu na kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,.
Picha: Rena
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, akimsikiliza mbunifu wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa COSTECH Dk. Amos Nungu na kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,.

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ina majukumu ya kitaifa kusaidia wabunifu na watafiti nchini hususani wanaochipukia, wachangie hatua za maendeleo kitaifa katika eneo hilo, wao na nchi kutambulika kitaifa na kimataifa.

Moja ya eneo linalochukuliwa nalo, ni kupitia makongamano ya wabunifu na watafiti kwa nyakati tofauti, hata kuchochea ushawishi wa vijana kuwasilisha mawazo yao ya kibunifu, ili yaboreshwe na kutambulika ndani na nje ya nchi. 

Makongamano hayo yamekuwa kichocheo kikubwa kwa wabunifu kupanua wigo na fikra za teknolojia za kisasa, hata wanatatua changamoto za kimaendeleo, hususani kwenye miradi inayotekelezwa katika maeneo tofauti. 

Hivi karibuni kulikuwapo kongamano lililoshirikisha wabunifu na watafiti kutoka maeneo mbalimbali nchini, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam. 

Mfunguzi wa kongamano, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko, akalenga zaidi kuwatambua watafiti waliofanya vizuri kwenye tafiti zao ndani na nje ya nchi. 

Hapo yupo Angelina Silvester, mbunifu na mwanzilishi wa Kiwanda cha Kutengeneza mvinyo kwa kutumia zao la nyanya.

 Hapo anasafiri na hoja ya mikakati hiyo, akisema imekuwa msaada mkubwa unaowanyanyua wabunifu, ili kazi zao zitambulike ndani ya jamii na nje. 

Kutokana na hilo, Mtafiti huyo anasema, vijana wenye mawazo chanya ya kubuni teknolojia yoyote, kwa ajili ya kuleta maendeleo wasibweteke na mawazo yao, bali wayawasilishe COSTECH ili yaweze kufanyiwa kazi na kuleta matokeo kwao na taifa kwa ujumla.

 Anashauri kuwa, mtu akiwa na wazo lake aanze kwanza kulifanyia kazi na baadaye awasilishe katika sehemu husika kiserikali, ili liboreshwe kwa kuleta matokeo chanya kijamii, pia kusaidia kumuinua kiuchumi mbunifu.

 "Nawashukuru sana COSTECH kutokana na fedha walizonipa kuendeleza teknolojia yangu ya kutengeneza ‘wine’ kwa kutumia zao la nyanya,"anatamka Angelina.

 DK AMOS NUNGU 

Dk. Amos Nungu, Mkurugenzi wa COSTECH, anasifu kongamano husika inaonesha Tanzania inaendeleza jitihada za kukuza utafiti wa kisayansi, maendeleo ya kiteknolojia na ubunifu, kama msingi wa maendeleo endelevu kiuchumi. 

 Anataja serikali imefadhili miradi kadhaa katika nyanja mbalimbali za utafiti, zikiwamo kilimo kupitia teknolojia za kisasa za kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula, afya kwa ubunifu wa tiba za magonjwa sugu na teknolojia za uchunguzi, ili kutoa suluhisho la utatuzi wa changamoto za kimaendeleo. 

Mkurugenzi Dk Nungu, anaeleza kwamba, uwekezaji huo unalenga kuwapa wanasayansi nyenzo na miundombinu inayohitajika, ili kufanikisha ubunifu unaobadilisha maisha ya Watanzania, wakiwamo vijana watakaochangamka kutumia changamoto, kuzigeuza fursa. 

Anasema ni mafanikio yanayoonekana, kutokana na ruzuku hizo zinazoleta matokeo chanya, ikiwamo kuongezeka utafiti wa kisayansi, ambayo kwa kiasi, inafungua nafasi za ajira hasa kwa vijana, pia fursa kwa watafiti na wabunifu vijana. 

 Anasema, katika kushirikisha jamii, miradi mingi imejikita kuwahusisha wananchi moja kwa moja, kuhakikisha matokeo yanawiana na mahitaji halisi ya jamii.

 WAZIRI WA ELIMU 

  Profesa Aldolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia, anasema serikali itaanza kuzitambua tafiti zinazofanyika kila mwaka, ikiwamo kuwatambua watafiti na kuwaongezea chachu ya ushawishi.

 Anasema, wameamua kufanya hivyo kuongeza hamasa katika ufanyaji tafiti, pia kujua umuhimu wa watafiti wanaoleta tija kulingana na utafiti wao.

 Waziri huyo anataja mfano  kumrejea wasomi wenzake, akiwataja kwa jina moja, watafiti maprofesa; Manji na Misinzo,  wakiendelea kutambua watafiti wengine.

 Hilo Waziri anasema, wameshafanya tafiti zilizosaidia kutatua changamoto kwa taifa, kwamba kila mwaka inasaidia kazi za nchi kujulikana ndani na nje ya nchi.

 DK. DOTO BITEKO 

Naibu Waziri Mkuu, ambaye ana dhamana ya Waziri wa Nishati, Doto Biteko, anasema watafiti na wabunifu wa ndani nchini, wanapaswa kutambuliwa na kupewa fursa ya kuchangia maendeleo ya taifa.

 Hapo anasisitiza kuwa, ili Tanzania ifikie malengo yake ya kiuchumi na kisayansi, ni muhimu kutambua na kuwekeza katika ubunifu wa wanasayansi wa ndani, ambao ndio msingi wa maendeleo endelevu. 

 Dk. Biteko anasema serikali imejizatiti kuwapa wanasayansi na wabunifu wa ndani nafasi ya kuleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali, zikiwamo kilimo, afya, nishati na usafiri. 

 Anafafanua kuwa, kupitia utafiti na ubunifu, watafiti wataweza kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi zinazokabili taifa, hivyo inachochea maendeleo. 

 Dk. Biteko anasema, watafiti na wabunifu wa ndani wanahitaji kutambuliwa kama sehemu muhimu ya mageuzi ya kijamii na kiuchumi na serikali imejizatiti kutoa mazingira bora ya kufanya tafiti na ubunifu kwa kuweka sera rafiki kwa wanasayansi, kuongeza rasilimali za kifedha na kuhakikisha kuwa miundombinu ya utafiti inaboreshwa ili kuwezesha tafiti za kisayansi. 

 “Watafiti wa Tanzania wanapaswa kuwa na fursa ya kutumia uwezo wao kubuni suluhu za kisayansi ambazo zitakuwa na manufaa kwa taifa, hivyo tutahakikisha kuwa tunawawezesha kufanya tafiti ambazo zitasaidia kuimarisha kilimo, kuboresha huduma za afya, na kutoa ufumbuzi wa nishati endelevu,” anasema Dkt. Biteko. 

 Anafafanua kuwa, COSTECH imeanzisha mifumo ya kutoa ufadhili wa tafiti na kutoa msaada kwa wabunifu wa teknolojia, ili kuongeza ubora wa tafiti zinazofanyika nchini ili kuwawezesha wanasayansi na wabunifu kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi

 Pia, imetenga fedha za kuanzisha na kuendeleza taasisi za utafiti, ikitoa vifaa vya kisasa vya kufanya tafiti.

 Hiyo ni pamoja na kuhamasisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, ili kubuni na kuendeleza teknolojia za kisasa zinazoweza kutatua matatizo ya jamii. 

 Katika kuimarisha uwezo wa wanafunzi na vijana, Dk. Biteko anaeleza ni muhimu kwa Tanzania kuongeza uwekezaji katika elimu ya sayansi na teknolojia, hasa kwa vijana na wanawake, ili kuwapa ujuzi na mitaji ya kuwa wabunifu wa baadaye.