WENYEJI Timu ya Soka ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), inatarajia kuikaribisha Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), katika mechi ya ufunguzi ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup 2025), itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Mashindano hayo mwaka huu yanashirikisha timu za taifa badala ya klabu kama ilivyozoeleka, na mataifa yaliyothibitisha kuleta vikosi vyao wanatumia michuano hiyo kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Kocha Msaidizi wa Zanzibar Heroes, Ali Suleiman Mtuli, alisema jana wamejiandaa vyema kuelekea mashindano hayo na wanaamini huu ni wakati wao wa kuwapa furaha Wazanzibar.
Mtuli alisema wachezaji wake wako tayari na mechi hiyo ya ufunguzi na itakuwa ngumu kutokana na historia ya timu hizo zinazokutana.
"Tunajua itakuwa mechi ngumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi siku ya kesho (leo), Mechi yetu na Tanzania Bara haijawahi kuwa rahisi kuanzia mashabiki mpaka wachezaji," alisema Mtuli.
Naye nahodha msaidizi wa timu hiyo, Ahmed Ali Suleiman 'Salula', alisema wachezaji wako tayari kwa ajili ya kupeperusha vyema bendera ya Zanzibar katika michuano hiyo.
Alisema kikosi chao kimepata muda mzuri wa kujiandaa na mashindano hayo na wanaamini hawatawaangusha mashabiki wao.
"Wachezaji tupo vizuri , hamasa ni kubwa kwetu na muda tuliopata wa kufanya mazoezi ya pamoja imekuwa ni sababu ya sisi kuwa na hamu ya kupata matokeo bora. Tuna deni kubwa kwa mashabiki wa Zanzibar Heroes, lakini niwaombe waje kwa wingi uwanjani kutupa hamasa zaidi ya kupata ushindi," Salula alisema.
Mashindano hayo yataendelea kesho kwa Kenya (Harambee Stars), kuikabili Burkina Faso na Januari 6, mwaka huu Burkina Faso itacheza dhidi ya Zanzibar Heroes na siku inayofuata Kilimanjaro Stars iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Hamad Ally, itawaalika Kenya.
Fainali za mashindano hayo zitafanyika Januari 13, mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED