Simba: Tuko salama Tunisia, tunajipanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:28 PM Jan 03 2025
Simba: Tuko salama  Tunisia, tunajipanga
Picha:Mtandao
Simba: Tuko salama Tunisia, tunajipanga

TOFAUTI na ilivyotarajiwa, uongozi wa Simba umesema msafara wao haujapata changamoto wala kufanyiwa figisu ya aina yoyote baada ya kuwasili nchini Tunisia kuwafuata wenyeji, CS Sfaxien kwa ajili ya mechi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, imethibitishwa.

CS Sfaxien itawakaribisha Simba katika mechi ya raundi ya nne ya Kundi A itakayochezwa keshokutwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania kwenye Uwanja wa  Olympique Hammadi Agrebi.

Katika mchezo uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, mashabiki wa CS Sfaxien walianzisha vurugu kufuatia Simba kupata bao la dakika za 'jioni' lililofungwa na Kibu Denis, wenyeji wakapata ushindi wa mabao 2-1, ambapo viti kadhaa vya uwanja huo viling'olewa.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wasiwe na wasiwasi wowote kwa sababu walitua Tunisia salama na hawakukutana na  changamoto yoyote kuanzia kwenye uwanja wa ndege hadi hotelini, sehemu ambazo mara nyingi dalili za figisu za soka huanzia hapo.

Ahmed alisema wamejitahidi kukwepa kila eneo ambalo wanadhani wangeweza kufanyiwa hujuma kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini Tunisia.

"Tumewasili salama baada ya safari ndefu, tumefika hapa hakuna changamoto yoyote, shauku imekuwa ni kubwa na hofu imekuwa kubwa hasa kwa Wanasimba wakioanisha na kile ambacho kilitokea katika mechi ya kwanza, pengine wakidhani ingeweza kutusumbua baada ya kufika hapa, niwaambie kila kitu kimekwenda vizuri.

Muda tuliokaa uwanja wa ndege ni ule ambao unatumiwa na viwanja vyote, maana yake hakukuwa na vigisu yoyote ile, lakini haya yote tumeyafanya kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Tunisia, kila kitu kimekwenda vizuri," alisema Ahmed.

Kuhusu hali ya hewa, Ahmed alisema ni baridi lakini siyo kama ile waliyokutana nayo nchini Algeria walipokwenda kucheza dhidi ya CS Constantine.

Naye nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri na wanatarajia kupambana kuhakikisha wanapata matokeo chanya.

"Tumekuja kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho ndani ya uwanja kwa dakika 90, hatuna hofu, mpaka sasa hakuna chochote, najua hakuna chochote kibaya kitakachotokea, pia sisi hatuogopi chochote, ni wazoefu sana katika michuano ya kimataifa na tumeshakutana na mambo mengi ndani na nje ya uwanja.

Sisi tumekuja kucheza mpira, hayo mambo mengine huwa yanatokea tu bila kupangwa, ukiangalia hata siku ile mashabiki wao walianzisha vurugu kwa sababu hawakupata matokeo waliyotarajia ya sare ambayo tayari wao walishajua wameipata," alisema beki huyo wa kushoto.

Hata hivyo, SC Sfaxien imepigwa marufuku kuingiza mashabiki kutokana na kufanya fujo katika mchezo wao dhidi ya CS Constantine ambao walipoteza kwa kufungwa bao 1-0, mechi iliyochezwa Novemba 27, mwaka jana.

Huenda klabu hiyo ikakumbana na rungu lingine kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kufuatia baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki kufanya vurugu katika mchezo dhidi ya Simba uliochezwa Desemba 15, mwaka jana.

Baada ya mechi hiyo, Simba itajipanga kuwafuata Bravos do Maquis na itamaliza mechi za hatua ya makundi nyumbani kwa kuwakaribisha CS Constantine kutoka Algeria.