TRA yaweka kambi Shinyanga, wafanyabiashara watoa ya moyoni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:22 PM Apr 23 2024
Afisa Mkuu Msimamiz wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lutufyo Mtafya, akitoa elimu kwa mfanyabiashara, Marik Nguti, ambae ni mfanyabiashara wa Geita aliyefika banda la TRA viwanja vya EPZ Bombambili mkoani Geita.
PICHA: MPIGA PICHA WETU
Afisa Mkuu Msimamiz wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lutufyo Mtafya, akitoa elimu kwa mfanyabiashara, Marik Nguti, ambae ni mfanyabiashara wa Geita aliyefika banda la TRA viwanja vya EPZ Bombambili mkoani Geita.

UMBALI wa kufuata huduma za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Shinyanga, umetajwa kuwa moja ya changamoto wanazopata wafanyabiashara, na hivyo kusababisha kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari, kupungua.

Hayo yameelezwa leo na baadhi ya wafanyabiashara mkoani hapa, baada ya timu ya maofisa kutoka TRA idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, kupiga kambi mkoani hapa, lengo likiwa ni kutoa elimu ya kodi.

Zoezi hilo walilolipa jina la 'mlango kwa mlango,' limalenga kuwafikia wafanyabiashara wa mijini na vijijini mkoani humo, mjini pamoja na vijijini.

Wafanyabiashara hao wamesema kuwa, wanapotaka huduma za TRA, wanalazimika kusafiri kwa masafa marefu kuzifuata, jambo linaloongeza gharama lakini pia likiwachukulia muda mwingi.

Mbali na kutoa elimu, zoezi hilo linafanyika sambamba na ukusanyaji wa maoni, changamoto na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara, lengo likiwa ni kutaka kufanya maboresho ya huduma za kikodi na hatimae kurahisisha ulipaji kodi kwa hiyari. 

Aidha, baadhi ya wafanyabiashara  wamefurahishwa na zoezi hilo ambalo limewasaidia kufahamu mambo mbali mbali ya kikodi, huku wakitaka zoezi hilo kuwa endelevu ili waendelee kujifunza zaidi.