HALMASHAURI ya Wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan imepokea Sh. bilioni 20 zilizotumika katika miradi mbalimbali ikiwemo ya afya na elimu.
Mkurugenzi wa Hamashauri ya Wilaya ya Makete, Willium Makufwe aliyasema hayo wakati akieleza mafanikio ya Rais Samia katika miaka mitatu ya uongozi wake.
Alisema hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa ofisi za kisasa za halmashauri na wamepokea shilingi bilioni mbili.
“Huu mradi tuafanya chini ya mkandarasi mjenzi MUST na mnaona hata tulivyoingia vifaa vya ujenzi vipo kwa hiyo ninachowaomba wenzetu wa MUST waongeze kasi ya ujenzi. Ni kweli Makete tunachangamoto ya mvua zinanyesha lakini watumie nafasi vizuri na wafanye kazi kwa tija ili jengo liweze kukamilika na kutoa huduma inayostahili,” alisema Makufwe.
Makufwe alisema miradi mingine ipo katika Shule ya Sekondari Iwawa, madarasa 12, Sekondari Usililo madarasa 12, Sekondari Mount Chafukwe madarasa 12.
“Katika kipindi cha miaka hii mitatu Rais Samia ameleta hapa zaidi ya Sh. bilioni 20 na kwa uchache tu tuna vituo vya afya karibia vitano kwa hiyo ninachowaomba wanamakete hasa wazazi na walezi lazima tuiunge mkono serikali” aliongeza Makufwe.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Makete, Dk. Jonathan Kitundu alisema katika kipindi cha miaka mitatu wamepata fedha kwa ajili ya ukarabati wa hospitali pamoja na ujenzi wa jengo la huduma za dharura.
Kwa upande wa sekta ya elimu miongoni mwa shule iliyopata maboresho makubwa ni pamoja na Shule ya Sekondari Lupalilo ambapo Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Kilatu alisema shule hiyo ilikuwa na changamoto kubwa kwenye miundombinu na kuwalazimu wazazi kuchangia mara kwa mara kwa ajili ya ujenzi.
Miongoni mwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lupalilo wakiwemo Respoka Mahenge na Leokadia Nyika walimshukuru Rais Samia kwa ujenzi wa miundombinu hiyo na kuahidi kwenda kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
Mmoja wa wakazi wilayani Makete, Daima Kilale alisema halmashauri hiyo imekuwa na maendeleo makubwa hususani kwenye maboresho ya miundombinu, huku wakibainisha kuwa awali katika maeneo mengi hususani kwenye Hospitali ya Wilaya ambapo vitanda vilikuwa vichache lakini pia visivyokuwa na ubora ukilinganisha na sasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED