DC Kissa awataka vijana kuchangamkia fursa Njombe

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 12:30 PM Apr 06 2024
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa.
Picha: Elizabeth John
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa.

MKUU wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa amewataka vijana kutoka mikoa yote hapa nchini, kufika Njombe kwa ajili ya kuangalia fursa zilizopo na kuzichangamkia ikiwa ni sehemu ya vijana kukabiliana na changamoto ya ajira iliyopo hapa nchini.

Wito huo umetolewa wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kongamano la vijana lililolenga kutafuta fursa za uwekezaji zitakazosaidia kuwakwamua vijana katika umasikini ambalo litafanyika wilayani Njombe.

Amesema wameamua kufanya kongamano hilo kwakua viongozi waliopo kwenye wilaya hiyo ni vijana na Rais amewapa fursa hivyo wameona ni vema kutumia nafasi zao katika kuwasaidia vijana wenzao.

Katibu tawala wilaya ya Njombe Agatha Mhaiki  amesema kwa wale watakaochagua fursa ya kilimo halmashauri zimejiandaa na kuna maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kilimo.

Mkuu wa idara ya kilimo na uvuvi Halmashauri ya Mji wa Makambako, Beatrice Tarimo amesema katika kuhakikisha kuwa mazao yatakayozalishwa na vijana hao yanapata masoko ya uhakika kwa mazao ya nafaka mahindi na mpunga serikali imetoa fursa ya ununuzi mazao kupitia wakala wa uhifadhi wa chakula (NFRA).

Kaimu afisa mipango halmashauri ya mji wa Makambako Nakembetwa Makala amesema halmashauri hiyo imetenga ekari 16 katika mtaa wa Idofi na majengo kwa ajili ya vijana kuwekeza viwanda pamoja na maghala.