Wachezaji wa CHAN waanze kuangaliwa sasa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:49 AM Sep 21 2024
Makamu wa 4 wa Rais wa CAF, Seidou Mbombo Njoya
Picha:Mtandao
Makamu wa 4 wa Rais wa CAF, Seidou Mbombo Njoya

TAYARI Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza tarehe za Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2025, itakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.

Makamu wa 4 wa Rais wa CAF, Seidou Mbombo Njoya, ambaye pia anahudumu kama Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) ndiye aliyetamka rasmi, Jumatatu iliyopita, mchana wakati wa mkutano na waandishi wa habari baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF jijini Nairobi nchini Kenya.

Itafanyika Februari 1 hadi 28 nchini Kenya, Uganda na Tanzania. Pia ilithibitishwa kuwa mechi za kufuzu kwa CHAN zitaanza kati ya Oktoba 25-27 na kumalizika Desemba mwaka huu kabla ya fainali hizo.

Nchini Tanzania serikali inaonekana kujiandaa kwa vitendo kwani tayari imeanza kujiandaa kwa miundombinu kwa kujenga viwanja vipya, kukarabati vilivyopo, kukarabati na baadhi ya viwanja ambavyo vitatumika kwa mazoezi.

Pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali kuzungumzia hilo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro, na naibu wake Hamisi Mwinjuma, lakini hata kwa macho vitendo vinaonekana kuwa nchi inapambana kwa ajili hiyo.

Na hii ya CHAN ni kama majaribio ya michuano ya AFCON ambayo Tanzania ni mwenyeji wake 2027, kwa ushirikiano wa Kenya na Uganda.

CAF wamezipa nchi hizi CHAN, ikiwa ni kama majaribio ya AFCON, ambayo huchezwa kwa wachezaji wote wanaocheza ndani na nje ya nchi.

Wakati serikali ikipambana, upande wa ufundi nao inabidi upambane kuangalia wachezaji bora ambao wanaweza kuiwakilisha nchi katika michuano ya CHAN.

Kwa sababu CHAN ni michuano ya wachezaji wa ndani, ina maana inawashirikisha wachezaji wale tu wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara, au Championship.

Ushauri wangu ni kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), linatakiwa kuwawezesha makocha wa timu za taifa, Hemed Suleiman 'Morocco' na mwenzake Juma Mgunda kuzunguka nchi nzima kuangalia michezo mbalimbali ya Ligi Kuu ili kuangalia wachezaji watakaokuwa kwenye kikosi hicho.

Pamoja na kwamba klabu za Simba, Yanga na Azam wana wachezaji wa Kitanzania bora, lakini tusiendelee kukariri kwamba katika klabu zingine hakuna wachezaji wazuri.

Kwa sababu michuano ya CHAN haiwahusu wachezaji wa nje, kuwe na wigo wa kuwapata wachezaji wengine bora kutoka klabu zingine.

Ukitaka kujua wachezaji wazuri wapo, ila kuna tatizo la kuwatambua, kila msimu klabu za Simba na Yanga zinasajili kutoka klabu hizo hizo za chini. Wakati mwingine mpaka zile timu ambazo zimeshuka daraja.

Sasa unashangaa Kamati za Ufundi za TFF inashindwa vipi kuwawezesha makocha wake kusaka wachezaji wengine wazuri mikoani kutoka klabu mbalimbali nchini badala ya kujaza wa Simba na Yanga na Azam tu kwenye kikosi.

Februari mwakani si mbali, hivyo kazi hiyo ianze sasa. wakati serikali inaendelea na mchakato wa viwanja na miundombinu, TFF nayo ianze kazi ya kuanndaa wachezaji kwa kuwaangalia wanaofaa kuchezea timu ya taifa kwenye michuano ya CHAN, wakati Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea.