Serikali kujenga shule za ufundi 100

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:17 AM Sep 21 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda
Picha:Mtandao
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda

SERIKALI inajenga shule za sekondari za ufundi 100 nchi nzima ili kuwaandaa vijana kupambana katika sekta ya ajira.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alibainisha hayo wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa serikali mkoani Njombe.

Alisema kuwa kwa mkoa wa Njombe, shule hiyo maalum ya sekondari itajengwa eneo lililotengwa katika Kijiji cha Magoda lenye ukubwa wa ekari 26.

Prof. Mkenda alisema serikali imeanzisha miradi, ikiwamo kwenye sekta za afya, elimu na maji ambako kote fedha zimekwenda ili kuikamilisha na kuwaondolea adha wananchi.

"Kuna barabara, bado tumepewa fursa ya kujenga shule amali za mrengo wa ufundi kwa sababu amali ni ufundi na ufundi stadi," alisema Prof. Mkenda.

Waziri huyo aliwataka watumishi wa serikali mkoani humo kutoona haya kueleza mafanikio ya serikali katika utekelezaji miradi ya maendeleo.

"Rais huyu (Samia Suluhu Hassan) tunajua ameanza kuingia makubaliano ya kurudisha hadhi ya reli ya Tazara ifanye kazi kama inavyotakiwa, tuanze kulima vizuri maparachichi kwa sababu miundombinu imeboreshwa," alisema Prof. Mkenda.

Alisema kuwa hivi sasa serikali itahakikisha kila mtoto anakwenda shule ya sekondari na msingi kwa sababu hakuna ada na itaendelea kuboresha miundombinu kuwa ya kisasa.

Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari alisema kuwa katika sekta ya elimu, mkoa huo umepokea Sh. bilioni 58.4 kwa ajili ya uwezeshaji huduma za elimu ukiwamo ujenzi wa miundombinu ya madarasa na mabweni.

Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika alisema serikali imeleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo ya sekta ya maji.

Alisema mradi wa maji miji 28 wenye thamani ya Sh. bilioni 40 ambao utasaidia kutatua tatizo la maji mjini Njombe.

Baadhi ya wananchi mjini Njombe, akiwamo Aghata Mfuji, walisema ujenzi wa shule hizo utasaidia kuwapa vijana elimu itakayowasaidia katika maisha yao kwa kuwa na ujuzi ambao utawasaidia kupata ajira.