CCM yasisitiza uhusiano wa Kimataifa, kuimarisha uchumi na maendeleo ya watu

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 11:18 AM Sep 20 2024
CCM yasisitiza uhusiano wa Kimataifa, kuimarisha uchumi na maendeleo ya watu
Picha:Mpigapicha Wetu
CCM yasisitiza uhusiano wa Kimataifa, kuimarisha uchumi na maendeleo ya watu

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka msisitizo katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa wenye manufaa ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Alisema kuwa urafiki na uhusiano wa kidiplomasia unapaswa kuendelea kuwa mojawapo ya njia sahihi katika kuboresha ushirikiano wa pande mbili kimataifa, kati ya nchi na nchi, au nchi na majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Alisema hayo jana alipokutana na mabalozi wanaowakilishi nchi zao hapa nchini, kutoka nchi za Brazil na India, pamoja na Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje ya Chama Tawala cha Msumbiji (FRELIMO) na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES), nchini Tanzania.

Katika mazungumzo na viongozi hao, yaliyofanyika kwa nyakati tofauti tofauti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, Balozi Nchimbi alsema mojawapo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM unaofanywa na Serikali ya CCM ni pamoja na kuendelea kuboresha uhusiano wa kimataifa, hasa kupitia diplomasia ya uchumi, kwa ajili ya kuimarisha uchumi, maendeleo ya watu na kubadilishana uzoefu kwenye uongozi na demokrasia.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Gustavo Martins Nogueira na Balozi Nchimbi, viongozi wote wawili walionesha msisitizo na utayari wa kuendelea kuboresha uhusiano kati ya Tanzania na Brazil kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili, hasa katika nyanja za afya, kilimo na michezo.

Kwenye mazungumzo ya Balozi Nchimbi na Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey, viongozi hao wamezungumzia umuhimu wa kuendelea kuenzi ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali, zikiwemo teknolojia, biashara na elimu, ikizingatiwa India ni mojawapo ya nchi zilizopiga hatua kubwa za kimaendeleo katika maeneo hayo