Kocha Mgunda anukia KenGold

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:57 AM Sep 20 2024
KOCHA wa zamani wa klabu ya Simba, Juma Mgunda
Picha: Mtandao
KOCHA wa zamani wa klabu ya Simba, Juma Mgunda

KOCHA wa zamani wa klabu ya Simba, Juma Mgunda anatajwa kuwa mmoja wa makocha 10 waliopeleka wasifu wao kwenye klabu ya KenGold kutaka kuirithi kazi ya Fikiri Elias aliyejiuzulu wiki hii kwa kile alichodai kushindwa kutimiza malengo.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa tayari makocha mbalimbali nchini wameshapeleka maombi ya kuitaka kazi hiyo, akiwemo Mgunda ambaye hivi karibuni alimaliza mkataba na klabu ya Simba akiwa amezifundisha timu za wanaume na wanawake.

Taarifa zinasema kuwa baadhi ya makocha ambao wametuma wasifu wao kutaka kuifundisha timu hiyo iliyoanza kucheza Ligi Kuu msimu huu ni pamoja na Zuberi Katwila, Fransis Baraza, Malale Hamsini na Mrundi, Haruna Hermana.

Hivi karibuni pia kulikuwa na taarifa ya Mgunda kutakiwa na Namungo baada ya timu hiyo kuwa na matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi Kuu huku kukiwa na tetesi za kutaka kuachana na kocha wake Mwinyi Zahera.

Kocha Elias alijiuluzu Jumatatu iliyopita mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC na kuchapwa bao 1-0, mchezo huo ulichezwa Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

"Nilijiwekea malengo kuwa nisipopata pointi sita katika michezo minne basi nitajiuluzu, sasa tayari mchezo wa tatu hatujapata pointi hata moja, na hata kama nikiendelea na kushinda tunakuwa na pointi tatu. Mimi kama mwana taaluma, nimefanya hivi kulinda taaluma yangu pamoja na uwajibikaji," alisema kocha huyo wakati akitangaza kujiuzulu.

Kilikuwa ni kipigo cha tatu mfululizo kwa timu hiyo ambayo mwanzo ilichapwa mabao 3-1 dhidi ya Singida Black Stars, ikafungwa mabao 2-1 dhidi ya Fountain Gate, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati Mkoani Manyara, kabla ya kipigo cha tatu kilichomfanya kocha huyo ajiuzulu.