Waamuzi wanne wasimamishwa Z'bar

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 11:02 AM Sep 20 2024
Waamuzi wanne wasimamishwa Z'bar
Picha:Mtandao
Waamuzi wanne wasimamishwa Z'bar

WAAMUZI wanne wanaochezesha Ligi Kuu ya Zanzibar wamesimamishwa katika ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitano baada ya kushindwa kutafsiri na kusimamia Sheria 17 za mpira wa miguu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamati ya Uendeshaji na usimamizi wa Ligi hiyo, waamuzi hao waliruhusu KMKM kuchezesha wachezaji 12 kwa muda wa dakika nne wakati timu hiyo ilipocheza na Muembe Makumbi. 

Taarifa hiyo ilieleza kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa sura ya 27 kifungu cha tatu ibara ndogo ya pili na tisa ya kanuni ya mashindano. 

Waamuzi walikumbana na adhabu hiyo ni mwamuzi wa kati Haji Nyonje na wasaidizi wake Yussuf Issa Shombe na Ismail Masoud Bakar na mwamuzi mezani Hamiar Muhsin Kamara wa mezani. 

Hivyo kamati hiyo inawashauri waamuzi hao kufuata kanuni na Sheria za soka, kuwa na utimamu na umakini wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, ili kulinda heshima ya mpira wa Zanzibar na makosa yasijirejee.

Sambamba na hayo kamati hiyo imetoa onyo kwa waamuzi Rashid Farahan, Haji Nyonje na Hamiar Muhsin Kamara kwa kushindwa kuwasilisha ripoti ya mchezo waliochezesha na kutojazwa kikamilifu na unadhifu na kwa waliotakiwa kuwasirisha ripoti ya mchezo kinyume na matakwa ya sura ya 27, kipengele cha pili, cha tatu na cha tano ya kanuni ya mashindano.

===