NMB yachochea moto mchezo wa Yanga, CBE

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:51 AM Sep 20 2024
Makamu wa Rais wa klabu ya Yanga, Arafat Ally Haji (kushoto), akimkabidhi jezi ya timu hiyo, Meneja Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Said Shaame (kulia) baada ya mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza wadhamini wa mechi ya marudiano
Picha:Mpigapicha Wetu
Makamu wa Rais wa klabu ya Yanga, Arafat Ally Haji (kushoto), akimkabidhi jezi ya timu hiyo, Meneja Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Said Shaame (kulia) baada ya mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza wadhamini wa mechi ya marudiano

WAKATI kikosi cha Yanga kikiwasili salama jana visiwani hapa kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE ya Ethiopia, benki ya NMB imekoleza moto kuelekea mchezo huo baada ya kutangaza kudhamini mtanange huo.

Yanga wanashuka uwanjani kesho saa 2:30 kuumana na mabingwa hao wa Ethiopia huku wakiitambulisha NMB kama mmoja wa wadhamini wa mchezo huo wakiupa jina la 'Timu Bora, Benki Bora'.

Akizungumza kwenye hafla ya utambulisho wa udhamini huo, Meneja Biashara wa benki hiyo Zanzibar, Naima Said Shaame, alisema siri ya uamuzi wao wa kujitosa kuidhamini Yanga ni mvuto ilionao klabu hiyo, unaoakisi mafanikio makubwa katika soka kitaifa na kimataifa.

“Tumevutiwa na mafanikio ya klabu hii, tukaona ipo haja ya Timu Bora kupewa nguvu na Benki Bora. Wametoka kutwaa Ngao ya Jamii katika ufunguzi wa msimu huu, lakini katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wamefuzu raundi hii kwa kishindo baada ya kuwachapa Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.

“Kwa kutambua ukubwa wa Yanga, tukalinganisha na ukubwa wa NMB, tukaona ipo haja ya kuwasapoti katika mechi dhidi ya CBE itakayopigwa hapa wikiendi hii na leo (jana) tuko hapa kutambulishwa rasmi kama washirika wa Yanga kuelekea mechi hii,” alisema Naima.

Alibainisha ya kwamba, ushirikiano baina ya benki yake na Yanga umeshaanza katika kuhanikiza wiki nzima na wanaamini mchango wa taasisi yake utakuwa chachu ya Yanga kushinda mechi hiyo na kufuzu hatua ya makundi kwa mara tatu katika historia yao.

“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha mashabiki wa Yanga kuwa, huu sio mwanzo, kwani tunafanya kazi na Yanga katika maeneo mbalimbali ikiwemo usajili wa wanachama kupitia kadi tofauti tofauti. Ukiona Tawi la NMB, maana yake umeiona Yanga na unaweza kusajili uanachama wako hapo.

Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, aliwashukuru NMB na wadhamini wenza kwa kuchagua kushirikiana na timu yake katika kuipa nguvu kuelekea hatua ya makundi ya michuano hiyo.

“Tunawashukuru NMB na wadhamini wengine wote waliowezesha wiki hii yote ya kujiandaa kuelekea mechi hii, mmeiheshimisha Yanga, kwani kabla hatujahesabu mauzo ya tiketi zetu za mechi, tayari tushaingiza zaidi ya Sh. Mil. 200 kutoka kwa wadhamini wetu hawa tu,” alitamba Kamwe.

Alibainisha ya kwamba ratiba ya matukio kwa Ijumaa hii yatafunguliwa kwa dua maalum itakayosomwa katika Madrassat Swifatul Nnabawwiyah iliyopo Kilimani kwa Msolopa, Zanzibar asubuhi na baada ya Swala ya Ijumaa, watatoa misaada kwa Watoto Yatima visiwani hapa.

“Tayari kikosi chetu chote kimetua Zanzibar kasoro Farid Mussa tu ambaye ni majeruhi na sababu za kusafiri na kikosi chote ni kundelea kujiandaa na mechi za ligi kuu zinazofuata, tuna ratiba ngumu mno ambayo hairuhusu mchezaji yeyote kuachwa mbali na kikosi," alisema Kamwe.

Yanga inahitaji sare au ushindi wowote kuweza kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Jumamosi iliyopita kuibuka na ushindi wa bao 1-0.