Mapya yaibuliwa tukio watu watatu kuuawa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 12:38 PM Sep 20 2024
   Mapya yaibuliwa tukio watu watatu kuuawa
Picha: Mtandao
Mapya yaibuliwa tukio watu watatu kuuawa

BABA wa familia ya watu watatu waliouawa na watu wasiojulikana katika Kata ya Nala, jijini Dodoma, Robert Mugema ameomba serikali kuimarisha ulinzi katika mtaa lilikotokea tukio hilo kwa kuwa kuna hofu.

Amesema kuwa siku watoto wake wanauawa, kuna taarifa kwamba baadhi ya nyumba za mtaa huo zilifungwa milango kwa makufuli. 

Septemba 16, mwaka huu, nyumbani kwa Mugema, waliuawa watu watatu ambao ni Milcah Robert (12), Fatuma Mohamed (20) na binti wa kazi, Makiwa Abdallah (16) huku mama wa familia hiyo, Lusajo Mwasonge (40) akijeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma. 

Akizungumza juzi nyumbani baada ya ibada ya kuaga mwili wa binti yake, Mugema alisema anakwenda mkoani Geita kwa ajili ya mazishi ya aliyekuwa mfanyakazi wake wa ndani, lakini familia yake itabaki katika nyumba hiyo. 

Hivyo, aliomba Serikali ya Mtaa, wilaya na mamlaka zote za ulinzi na usalama waendelee kuimarisha ulinzi mahali hapo kwa sababu bado hana imani. 

"Nina roho ya ujasiri ndani yangu lakini mwili wangu ni dhaifu sana, mnaponiona nalia si kuwa siwasikii mnaponihamasisha niwe imara. Moyoni mwangu niko imara kabisa lakini mwilini kwangu ni dhaifu sana, niwaombe kuimarishwe ulinzi katika maeneo ya Segu Bwawani. 

"Wakati wa tukio kuna baadhi ya majirani nyumba zao zilifungwa kwa makufuli, maana yake eneo hili haliko salama au halikuwa salama. Simlaumu mtu wala kumtaja yeyote lakini Mungu awabariki kwa mkono wake," alisema. 

Awali, akitoa mahubiri katika ibada ya kuaga miili, Askofu wa Kanisa la The Gospel Special Message Ministry (Gome), Majid Salim Ally, alisema tukio hilo ni baya na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kama ilivyo kwa matukio mengine. 

"Uovu unaangamiza nchi na ninatamka sasa hawa waliofanya tukio hili wakamatwe kwa jina la Yesu, niombe serikali iongeze nguvu kwenye vyombo vya ulinzi na usalama wasipewe taarifa na kukaa nazo bila kuzitendea haki," alisema. 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Segu Bwawani, Jeremiah Mulima alisema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alifika eneo la tukio na kuwaomba wananchi kuwa watulivu na kusubiri tamko la polisi ngazi ya wilaya na mkoa.