Warioba aonya mwelekeo wa siasa nchini

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 12:16 PM Sep 20 2024
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba
Picha:Mtandao
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ametahadharisha siasa nchini iko katika mwelekeo mbaya.

Amesema kuwa kwa miaka mingi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umekuwa unasimamiwa na serikali na umekuwa huru na haki, lakini alichokishuhudia mwaka 2019 ni kama nchi inarejea kwenye mfumo wa chama kimoja. 

Vilevile, ametoa angalizo kuwa siasa imegeuka kutoka kutoa hoja na kukosoana kwa lengo la kujenga nchi, hivi sasa anaona siasa za ukabila na udini. 

Jaji mstaafu Warioba aliyasema hayo jana wakati wa mkutano wa Kituo cha Demokrasia (TCD) na wadau waliokutana kujadili tathmini ya hali ya demokrasia nchini mkoani Dar es Salaam jana. 

Alisema Uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za Mitaa utakuwa na umuhimu mkubwa kulinda amani ya nchi, akishauri kufanyike tathmini ya utawala bora na demokrasia. 

"Mjue uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na umuhimu mkubwa kwa amani ya nchi yetu. Lazima tutafute njia ambayo itafanya sote tutaridhika. 

"Bado mpaka jana nilikuwa ninajitahidi, bado muda mfupi tunakwenda Uchaguzi wa Serikali za Mtaa, tutafakari viongozi wote tunaohusika tukubaliane, tutakapokwenda katika uchaguzi tuwe tumekubaliana, la sivyo tukienda na mapambano haya, yanaweza kujenga misingi ya vurugu katika nchi yetu. 

"Mambo ya msingi ndiyo yanayosababisha vurugu na tusisahau tuna uzoefu katika nchi hii yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001, tusije tukafika katika hali hiyo," alionya. 

Jaji Warioba aliongeza: "Siku hizi ukizungumzia demorasia ndani ya Tanzania ni kama unazungumzia ilianza miaka 30 iliyopita baada ya mfumo wa vyama vingi, ninadhani hapo tunakosea, tuanzie mbali zaidi.

 "Katiba inasema msingi wa madaraka na mamlaka ni wa wananchi (Ibara ya 8 ya Katiba ya nchi), kimsingi unapozungumzia demokrasia unazungumzia wananchi. Katika tathmini tuangalie wananchi wamefaidika vipi," alisema.

 Jaji Warioba alisema wao walioishi wakati wa ukoloni, hakukuwa na demokrasia, na sasa wanazungumzia uhuru wa kutoa mawazo, kusikika, mikutano ya hadhara na maandamano.

 "Wakati ule hakukuwapo hivyo, wakati wa wakoloni pamoja na sasa ndio wale ambao walikuwa hapa wakaona demokrasia hapa haifai, sasa ndio wamekuwa mafundi wa kutufundisha demokrasia.

 "Tujiulize mnapofanya tathmini wananchi wana haki ya kuchagua wawakilishi wao? Eneo moja mngefanya utafiti mwone wananchi wanaonesha vipi, mwone wanavyojitokeza kupiga kura.

 "Mwangalie wakati wa mfumo wa chama kimoja wakati wa uchaguzi wananchi walikuwa wanajitokeza kwa wingi  2019/20 ilikuwa ajali, haikuwa katika utaratibu wa kawaida wa mchakato wa uchaguzi. 

 "Kila uchaguzi una dosari, hakuna unaoweza kupita bila dosari, lakini mawakala walisambaratishwa wengi tu, hata upigaji kura wenyewe halikuwa jambo la kawaida."

 Alisema kuwa hivi sasa anadhani ugomvi mkubwa ni waliosimamia uchaguzi 2019/20 ndio wataendelea kusimamia.

 "Wanaaminika? Ninajiuliza, ukichukua mfano Serikali za Mitaa, tangu wakati wa chama kimoja hadi mfumo wa vyama vingi, uchaguzi huu ulisimamiwa na serikali.

 "Mwaka 1994 ulisimamiwa na serikali, 1999, 2004, 2009, 2014, mara tano tumefanya Uchaguzi Serikali za Mitaa ukisimamiwa na serikali, kulikuwa na dosari za hapa na pale, lakini kwa ujumla ulikuwa wa haki na huru, na katika kipindi kile hata vyama vya upinzani vilishika vijiji.

 "Lakini 2019 inabadilika kabisa, mwisho unakuta kama tumerudi mfumo wa chama kimoja. Kwanini ilitokea hivyo? Ninadhani hayo.

 "Mimi isingenipa tatizo, nimekuwa nikitetea mabadiliko ya katiba lakini bado niliamini tungeweza kufanya uchaguzi huru na haki, lakini sasa hivi ni ngumu," Jaji Warioba alisema.

 Waziri Mkuu mstaafu huyo aliweka wazi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na timu yake walifika nyumbani kwake kumsalimia na akajaribu kuwashawishi waahirishe maandamano. 

 Alisema kuwa aliwatafuta na upande wa pili, Chama Cha Mapinduzi (CCM), akawaambia amekaa na CHADEMA wamemweleza wasiwasi wao na ni vizuri washughulikiwe, akihakikishiwa uchaguzi utakuwa huru na haki.

 Alisema aliona matukio likiwamo la Mbeya, akajiuliza "Msajili wa Vyama vya Siasa ni mlezi wa vyama, hakuna njia ya mashauriano na kuleta suluhu?"

 Jaji Warioba alisema kuwa hivi sasa kwa lugha wanayozungumza, imefikia wananchi kuona ni mtu mmoja tu mwenye uwezo wa kufanya kila kitu, hata vijijini waandishi wa habari wakienda kuzungumza nao, wanasema tunaomba Rais atuangalie kwa jicho la tatu.

 "Tunafundisha demokrasia au usultani na ufalme? Ninadhani tathmini hizi tuzifanye. La mwisho, umoja na amani ya nchi; demokrasia katika nchi hii ni lazima uimarishe umoja na amani yetu, kama hailindi amani na umoja haitufai," alisema.

 MBOWE, LISSU

Mwenyekiti wa TCD, Mbowe, alisema mwezi Septemba umekuwa wa maombolezo kwa CHADEMA, akiwashukuru Watanzania wote, vyama vyote na taasisi mbalimbali ambao wamelia nao.

 "Kwetu ulikuwa mwezi mgumu mno, tunapata wakati mgumu kutafakari namna ya kufanya wajibu ulio bora ndani ya TCD na wakati huo tukilia kwa madhila tunayopata.

 "Ili demokrasia iwe na maana lazima itambue haki. Ili kuwa na demokrasia kwa taifa, lazima kuwe na utashi wa kisiasa na unatakiwa utoke kwa waliopewa dhamana kuongoza taifa," alisema.

 Alisema wamepoteza wenzao na kuendelea kutokujua wanachama na viongozi wenzao waliko. 

 "Nitambue katika mkutano huu, kumekuwa na upotevu wa viongozi wetu katika mazingira ya kutatanisha. Tumeomba serikali ituambie wako wapi, nao wanasema hawajui wako wapi. Basi sintofahamu inabaki kwa taifa zima," alisema.

 "Mnategemea taasisi mliyoisajili ifanye shughuli za kihalali za kisiasa ifanye nini? Tuna deni la roho za watu," alisema Mbowe.

 Katika mkutano huo, Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, alisema siku zote nchi yake imewekeza kwa watu na demokrasia, hivyo wanathamini mchakato wa demokrasia unaowahusu watu moja kwa moja.

 Alisema siku za hivi karibuni kuelekea katika uchaguzi, Tanzania na Marekani zimekabiliwa na vurugu ambazo zinatishia mchakato wa demokrasia katika mataifa hayo.

 Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu,  alisema kitu pekee kilichobadilika na cha maana kwa mtazamo wake katika sheria mpya ni kwamba, badala ya wagombea waliokuwa wanapita bila kupingwa, sasa sheria inasema wakienguliwa wakabaki peke yao, watapigiwa kura ya ndio au hapana.

 Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema: Yaliyotokea mwaka  2001 walipoitisha maandamano ya amani na watu kadhaa kupoteza maisha, hayapaswi kujirudia.

 Prof. Lipumba alisema maoni ya Jaji Warioba aliyotoa ni muhimu na kwa kuwa vyombo vya dola vipo, kuna haja kufanya mazungumzo na majadiliano ili mambo yasiharibike zaidi kuliko yalivyo sasa.

 Viongozi wengine waliohudhuriwa mkutano huo ni Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima.

 Wengine ni Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian Tanzania, Emmaus Mwamakula na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimam Tanzania, Shehe Issa Ponda.