Biteko azindua mradi umeme unaookoa bil. 19/- kila mwaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:47 PM Sep 20 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (kushoto) akiweka jiwe la msingi katika mradi wa Kufua Umeme Mto Malagarasi MW 49.5, mkoani Kigoma. Kulia ni Mkuu wa mkoa huo, Thobias Andengenye.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (kushoto) akiweka jiwe la msingi katika mradi wa Kufua Umeme Mto Malagarasi MW 49.5, mkoani Kigoma. Kulia ni Mkuu wa mkoa huo, Thobias Andengenye.

HISTORIA imeandikwa Kigoma baada ya kuwekwa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Malagarasi ambao utauwezesha mkoa kupata umeme wa gridi ya taifa.

Mbali na mradi huo, Kigoma pia itaanza kupata umeme wa gridi ya taifa katika njia zingine hali itajayowezesha kufungua zaidi mkoa kiuchumi. Umeme utakaozalishwa katika mradi huo utakuwa wa Megawati 49.5.  

Sambamba na mradi huo, pia limewekwa jiwe la msingi katika kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme katika eneo la Kidahwe, wilayani hapa.  

Akizungumza jana baada ya kuweka mawe hayo ya msingi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alisema hatua hiyo imeandika historia mpya katika mkoa wa Kigoma.  

Dk. Biteko alisema kutokana na hatua hiyo, Kigoma, moja ya mikoa ya pembezoni, sasa itageuka kuwa kitovu cha nishati na itakayofanya mkoa kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 

Alisema umeme huo na ule wa kutoka vyanzo vingine vya gridi ya taifa, vitafanya Kigoma kuwa na umeme wa uhakika ambao utachochea kasi ya maendeleo.  

"Kigoma sasa itafunguka kimaendeleo kwa sababu ya umeme wa gridi ya taifa. Baada ya kufunguka kwa miundombinu ya usafiri, sasa ni zamu ya kufunguka kwa umeme na hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali. 

"Enzi zile kabla ya barabara za lami, haikuwa shida ukiwa Mwanza au Dar es Salaam kumtambua mtu aliyekuwa akitoka Kigoma. Ulikuwa unamtambua kwa vumbi tu lakini sasa ni historia. 

"Sasa umeme wa uhakika wa gridi ya taifa unaanza kuingia Kigoma. Ile historia ya kuwa moja ya mikoa iliyo nyuma kiuchumi inafutika. Tulianza na barabara, tunakuja na umeme hatimaye treni ya kisasa (SGR). Nuru inawaka Kigoma," alisema. 

Naibu Waziri Mkuu Biteko alisema serikali imetoa Sh. trilioni 1.2 ambazo pamoja na ujenzi wa mradi wa Malagarasi, zitatumika kupokea, kupoza na kusafirisha umeme kutoka Nyakanazi kilovoti 620, ujenzi wa njia ya Tabora - Uvinza hadi Kigoma, Katavi hadi Uvinza kilovoti 220 kwa ajili ya treni ya SGR.  

Dk. Biteko alisema kuwapo umeme wa gridi ya taifa kutalipunguzia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) gharama za ununuzi wa mafuta mazito kwa ajili ya majereta yanayozalisha umeme.  

Kwa mujibu wa Dk. Biteko, kwa mwaka TANESCO hutumia Sh. bilioni 35 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kwa ajili ya kuzalisha umeme. 

"Pamoja na kutumia fedha hizo, ukiangalia kiasi kinachopatikana kwa ajili ya kuuza umeme ni Sh. bilioni 16, hivyo shirika linapata hasara ya Sh. bilioni 19. Kwa hiyo ulikuwa mzigo mkubwa na sasa tutauondoa," alisema.

 Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Boniface Nyamohanga, alisema Kigoma ilikuwa inapata Megawati 8.5 za umeme unaozalishwa kutokana na mafuta mazito na umeme wa jua Megawati 4.7 unaozalishwa na kampuni ya NextGen Solar.

 Alisema umeme wa gridi ya taifa utalipunguzia mzigo shirika wa uzalishaji na kuwa na umeme wa uhakika ambao utachochea kasi ya ukuaji uchumi wa mkoa, maisha bora ya wananchi na Pato la Taifa. 

 "Umeme huu pia utasaidia kuboresha huduma za kijamii kama elimu na afya. Pia utatengeneza ajira za muda mfupi na mrefu. Zaidi ya wafanyakazi 700 wanatarajiwa kuajiriwa.

 "Licha ya manufaa hayo, gharama za uzalishaji umeme zitapungua kwani tutaondoa majereta ambayo yalikuwa yakitumika kuzalisha umeme ambayo yalikuwa mzigo mkubwa kwa shirika," alisema.