Mchinjita atoa mbinu za kumaliza migogoro wafanyabiashara, serikali

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 01:05 PM Sep 20 2024
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita
Picha: Mtandao
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita ameshauri serikali inaposanifu na kujenga barabara, itenge maeneo kwa ajili ya machinga kufanya biashara zao ili kumaliza migogoro ya wafanyabiashara na serikali.

Mchinjita alishauri hayo jana Karume, jijini Dar es Salaam alipozungumza na wananchi, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zinazofanywa na viongozi wakubwa wa chama hicho waliojigawa kikanda.  

Ushauri mwingine aliotoa ni kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya machinga katikati ya jiji ili kupunguza mwingiliano wa kibiashara.  

Alisema hiyo itamaliza dhana ya kuonekana Kariakoo ni mahali pa mapambano kati ya wafanyabiashara na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). 

"Eneo la Kariakoo mizigo yake yote inatoka bandarini, serikali ilitangaze eneo la Kariakoo kuwa ni eneo huru la biashara. Hiyo itasaidia kuwaondoa maofisa wa TRA na huu mgogoro wa mara kwa mara hautatokea tena.

 "Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumeziba mwanya na kuondoa hali ya kuwindana na kuviziana kati ya wafanyabiashara na maofisa wa TRA," alisema Mchinjita. 

Kuhusu wananchi wanaoondolewa katika Bonde la Mto Msimbazi kulalamikia kutolipwa fedha kulingana na thamani ya eneo, alitaka serikali kurejea upya kwa wakazi hao kutatua changamoto hiyo. 

"Tunafahamu mradi wa Benki ya Dunia umetoa fedha zaidi ya Sh. bilioni 600 kwa ajili ya kubadilisha sura ya Bonde la Mto Msimbazi, lakini wananchi wanalipwa fedha kidogo. 

"Hata fidia wazolipa bado ni ndogo, kuna mama ameniambia yeye nyumba yake imebomolewa, analipwa fidia Sh. milioni 14 na hawajaambiwa kiwanja atapata wapi. 

"(Sh.) milioni 14 ni fedha ndogo sana kwa kiwanja kilichopo katikati ya jiji wakati leo ukivuka tu hapo Kigamboni kabla ya Mji Mwema kiwanja ni zaidi ya Sh. million 30," alisema kwa ukali Mchinjita. 

Alitaka serikali kurejea upya kinachoendelea katika bonde hilo na wananchi waliokataa kulipwa, waingizwe kama sehemu ya wanahisa ili wanufaike na mradi utakaojengwa. 

Akizungumzia ongezeko la machinga, Mchinjita alisema limetokana na seriali kutokuwa na mipango mizuri ya kuajiri vijana, akisistiza wengi wao ni waliohitimu vyuo vikuu na wakakosa ajira. 

Mchinjita alisema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kila mwaka vijana 1,000,000 wanaingia katika soko la ajira, lakini serikali huajiri vijana 70,000 tu, hivyo 930,000 hukosa ajira kila mwaka. 

Alisema hali hiyo imesababishwa na serikali kwa kutokuwa na ubunifu wa kuwawezesha vijana kupata ajira na kujiondoa katika lindi la umaskini. 

Akihitimisha mkutano wake kwa kuwataka wananchi kuunga mkono chama chake kwa kuwachagua viongozi wao ili waje na mbinu mbadala za kufanye kile alichokiita "kukomboa nchi".