Kafulila aipongeza CBE kwa ubunifu

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 02:12 PM Sep 20 2024
KAMISHNA wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila
Picha: Mpigapicha Wetu
KAMISHNA wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila

KAMISHNA wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila, amevitaka vyuo vya umma nchini kutumia sekta binafsi kujenga mabweni na miradi mbalimbali kwa ubia na sekta binafsi bila kutegemea fedha za Serikali.

Amesema miradi ya ubia inainufaisha zaidi serikali kwani inapata teknolojia mpya na za kisasa kutoka sekta binafsi na kusaidia uchumi wake kuendeshwa kisasa zaidi na kwa ufanisi.

Ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa chuo hicho kilichojadili utekelezaji wa mradi wa ubia wa ujenzi wa mabweni yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 12,000.

“CBE imeonyesha njia,  imetengeneza template  ambayo vyuo vingine vinapaswa kuiga  kwa kujenga mabweni  kwa ubia bila kuomba Hazina fedha za uendeshaji,” amesema Kafulila.

Amesema mamlaka zote za serikali zinazotekeleza miradi mbalimbali ziangalie uwezekano wa kuhusisha sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi hiyo badala ya kusubiri fedha za serikali.

Amesema kila mradi ambao sekta binafsi inaweza kuutekeleza ni vyema taasisi za serikali zikaingia ubia nazo ili kuharakisha utekelezaji wake na kuokoa fedha za serikali ambazo zingetumika.

“Kila mradi ambao sekta binafsi inaweza kuutekeleza kwa teknolojia ya hali ya juu kuliko serikali basi apewe autekeleze ili tujenge uchumi wa kisasa ambao sekta binafsi ndiyo inanafasi kubwa ya kutengeneza ajira nyingi,” amesema

Ameipongeza menejimenti ya CBE kwa kuratibu mradi wa ujenzi wa mabweni hayo ambayo yatakapokamilika yataondoa uhaba wa makazi ya wanafunzi kwenye kampasi  ya chuo hicho hapa jijini Dar es Salaam.

1

Kafulila amesema serikali iliamua kuweka utaratibu wa kuweka miradi kwa ubia ili kunufaika na mambo manne ikiwemo kutekeleza miradi yake bila kutumia fedha zake au mikopo kutoka mataifa ya nje.

“Utaratibu wa ubia unaleta unafuu kwa serikali kwasababu miradi inajengwa bila kutegemea fedha zake lakini utaratibu huu wa ubia unafanya serikali ivute teknolojia ya kujenga baadhi ya miradi, teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa inapatikana sekta binafsi,” amesema

Amesema kwa utaratibu wa ubia serikali inanufaika na teknolojia ya kisasa ambayo inapatikana kwenye sekta binafsi na kupata fursa ya kuleta weledi kwenye taasisi zake kama CBE.

“Kwa mfano mabweni haya yatakapojengwa na kukamilika mwekezaji atalipa kodi kwa serikali lakini kama ingejenga yenyewe ingekuwa huduma tu na hakuna kodi ambayo serikali ingepata kwa hiyo utaratibu huu unainufaisha sana serikali,” amesema.

Mkuu wa chuo hicho, Proesa Edda Lwoga, amesema mabweni hayo yatakayojengwa kwenye kampasi kuu ya Dar  es Salaam yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,728 hivyo  kupunguza pengo kubwa la malazi kwa wanafunzi.
2

Amesema kwa sasa kampasi ya CBE Dar es Salaam ina jumla ya wanafunzi 12,000, ambapo kwa upande wa malazi kampasi ina majengo mawili tu ya bweni  yenye uwezo wa kuchukua vitanda 160 pekee vya malazi kwa wanafunzi wa kike na kiume hivyo vinakidhi uhitaji wa malazi kwa asilimia 1.3 tu.

Mkuu wa chuo amesema mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kupunguza changamoto ya malazi kutoka asilimia  1.34 iliyopo mpaka asilimia 30  ya mahitaji ya wanafunzi kwa bweni.

“Hali iyopo imesababisha uhitaji mkubwa wa malazi ya wanafunzi kwa asilimia 98.6 hivyo wengi wanalazimika kutafuta malazi nje ya chuo kwa gharama kubwa, jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama hizo,” amesema.

3