Hospitali binafsi walalamika kucheleweshwa malipo bima afya

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:33 PM Sep 20 2024
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Cardinal Rugambwa, Dk. Jane Manyahi, watatu kushoto na Askofu Mkuu Msaidizi Jimbo la Dar es Salaam Hendry Mchamungu, wapili kulia wakiwa wameshika chetu baada ya kukabidhiwa.
Picha: Maulid Mmbaga.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Cardinal Rugambwa, Dk. Jane Manyahi, watatu kushoto na Askofu Mkuu Msaidizi Jimbo la Dar es Salaam Hendry Mchamungu, wapili kulia wakiwa wameshika chetu baada ya kukabidhiwa.

WADAU wa afya kutoka sekta binafsi wamesema kucheleweshwa kwa malipo yanayotokana na huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotibiwa kwa bima ya afya ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazowakabili na kusababisha kushindwa kutoa huduma kwa ufanisi.

Hayo yalibainishwa leo mkoani Dar es Salaam na Mganga Mfawidhi Hospital ya Cardinal Rugambwa, Dk. Jane Manyahi, wakati wa hafla ya kukabidhiwa cheti cha ufanisi wa huduma, kutoka taasisi ya 'Farm access' chini ya mpango wa 'Safecare' inayosimamia ufanisi wa utoaji huduma za afya kwa umma.

Dk. Jane ambaye ni bingwa wa magonjwa ya kina Mama na uzazi, amesema mkataba wao na bima mbalimbali za afya ni kulipwa ndani ya siku 90 lakini wakati mwingine inapitiliza mpaka siku 120 bila malipo wakati tayari wameshatoa huduma kwa wagonjwa.

"Tumekuwa na vikao mbalimbaki kupitia viongozi wetu kwaajili ya kuongea na watu wa bima za afya, hiyo imeleta unafuu kidogo, ingawa bado hatujaweza kulipwa kwa wakati unaopaswa na bado mazungumzo yanaendelea.

"Kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TRA) tuliomba kuwe na mtu ambaye atakuwa 'Moderator' kati yetu watoa huduma na bima za afya, ili kunapokuwa na matatizo awepo mtu anaetuweka pamoja na kuweza kutatua changamoto zetu," amesema Dk. Jane.

Ameongeza kuwa baada ya kupaza sauti kwa muda mrefu kwa sasa taasisi hizo za bima zimeanza kuwasikia na kuanza kupunguza siku za ulipaji, ingawa bado hawajafikia kiwango wanachokihitaji, cha ulipaji kwa wakati.

Amesema asilimia 90 ya wagonjwa wanaowahudumia niwa wateja wa bima ya afya, akieleza kuwa kama hawana mtaji wa kujiendesha kwa miezi mitatu hadi minne wanayokaa bila malipo, huduma zitakwama.

Akizungumzia cheti cha nyota tano walichotunukiwa, amesema kupata tuzo huo sio rahisi na ilikuwa ni mchakato wa muda mrefu, na kwamba wataendelea kusimamiana na kushirikiana katika vitengo mbalimbali katika kuhakikisha ufanisi na ubora wa huduma unaendelea kuwa kipaumbeli chao.