Kunenge atoa maagizo ujenzi bwalo la Shule ya Sekondari Bibi Titi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:23 PM Sep 20 2024
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amefanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Rufiji kukagua ujenzi wa bwalo la chakula Shule ya Sekondari ya Wasichana Bibi Titi pamoja na ujenzi wa barabara ya Nyamwage -Utete.

Akiwa katika shule hiyo Kunenge amewataka wakandarasi kuhakikisha bwalo hilo linakamilika kwa wakati na ubora unatakiwa. 

Kunenge amesema mkandarasi wa bwalo hilo anatakiwa kukamilisha kazi yake Septemba 30 kama alivyoahidi Ili wanafunzi waanze kutumia bwalo hilo na kwamba kama kuna msaada wa wataalamu unagitajika anatakiwa kutoa taarifa mapema.

" Bwalo linaridhisha tatizo ni kasi, tumewaambia haturidhiki na kasi wajipange vizuri wahakikishe Septemba 30 limekamilika," amesema 

Wakati huo huo Kunenge amefanya ukaguzi wa Barabara ya Nyamwage Utete km 33.7 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya zaidi ya sh. Biln 43 .

Mkuu huyo wa Mkoa amesema barabara hiyo ambayo inajengwa na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group (CRSG) anatakiwa kuweka mkakati wa kuukamilisha kulingana na muda uliopangwa.

1

" Hatutaki Rais Samia Suluhu Hassan aje hapa apokee malalamiko ya wananchi kuchelewa kwa barabara hii fanyeni kazi kwa ubora  na muikamilishe kwa wakati," amesema 

Awali mkaguzi wa barabara kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Joseph Chuwa alisema mradi huo kwasasa umefikia asilimia 5.01 kwa kiasi kinachokadiriwa kufikia sh. Biln 1.9 na kwamba miezi 14 imepita tangu kuanza huku kukiwa na upotevu wa asilimia 53 ya muda ukilinganisha na miezi kumi iliyobaki.

Kukamilika kwa barabara hiyokutaboresha usafirishaji bidhaa za viwandani kutoka Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Rufiji kwenda mikoa ya Kaskazini ya Morogoro, Iringa, Mbeya na nchi jirani za Malawi na Zambia.