Wajipanga kuendesha baiskeli hadi Butiama kumuenzi Nyerere

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:14 PM Sep 20 2024
Mkuu wa Mahusiano ya Vyombo vya Habari Vodacom Tanzania,  Annette Kanora kushoto na Meneja wa Mahusiano na Chapa wa benki ya Stanbic Tanzania, Annette Nkini, wakibadilishana mikataba wakati wa kujiandaa na kampeni Twende Butiama.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mahusiano ya Vyombo vya Habari Vodacom Tanzania, Annette Kanora kushoto na Meneja wa Mahusiano na Chapa wa benki ya Stanbic Tanzania, Annette Nkini, wakibadilishana mikataba wakati wa kujiandaa na kampeni Twende Butiama.

KATIKA kuenzi mema aliyofanya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kampuni ya simu za mkononi Vodacom Tanzania na Benki ya Stanbic zimetangaza msafara wa baiskeli mpaka Butiama.

Msafara huo una lengo la kusaidia uboreshwaji huduma za afya, elimu, utunzaji mazingira, kuongeza uelewa wa kusoma na kuandika pamoja na kutoa ujuzi maalumu wa kuwawezesha wananchi kufanikiwa kiuchumi.

Hayo yalisemwa juzi mkoani Dar es Salaam na Mkuu wa Uhusiano ya Vyombo vya Habari wa Vodacom Tanzania, Annette Kanora.

"Kupitia ushirikiano huu, tutaweka msisitizo juu ya uhifadhi wa mazingira na huduma za afya na maendeleo ya jamii kiujumla kuendana na maadili yaliyohimizwa na Mwalimu Nyerere. 

"Ziara hii itajumuisha shughuli mbalimbali, zikiwamo warsha za elimu, kambi za afya na kampeni za kuhamasisha uelewa wa mazingira, zikifikia jamii kote Tanzania.

"Ushirikiano huu unaonesha kujitolea kwetu kwa pamoja katika kuleta athari chanya za kijamii kote nchini. Kwa kuunganisha nguvu zetu, tunaweza kuendeleza maono ya Nyerere ya taifa lenye ustawi na ushirikishwaji," alisema Annette. 

Meneja Uhusiano na Chapa wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Nkini, alisema, "Kuwekeza katika elimu, afya na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni sehemu kuu ya uwekezaji wetu wa kijamii na juhudi endelevu. Tunafurahi kushirikiana na Vodacom kuleta athari chanya kwenye jamii."

Ziara hiyo itaanza rasmi Septemba 29 na itawakutanisha waendesha baiskeli ndani na nje ya nchi.