Mpanzu awasili nchini kumalizana na Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:24 PM Sep 20 2024
Elie Mpanzu
Picha:Mtandao
Elie Mpanzu

WAKATI timu yao ikitarajia kucheza mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli kesho, klabu ya Simba imemshusha winga, Elie Mpanzu nchini kwa ajili ya kumalizana naye kabla ya kumtangaza kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa Mpanzu aliwasili nchini juzi na tayari baadhi ya makubaliano yamefikiwa.

Imeelezwa kuwa Simba imekubali kutoa kiasi cha Dola za Marekani 200,000 ambazo ni sawa na kiasi cha Sh. Milioni 544 na atalipwa mshahara wa Sh. Milioni 27 kwa mwezi.

Awali mchezaji huyo ambaye anaichezea AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ilikuwa asajiliwe kipindi cha dirisha kubwa la usajili, lakini dili lilishikwa kufanikiwa, alipotimkia Klabu ya Genk ya Ubelgiji kwa majaribio, lakini mwisho wa siku alifeli.

Mtoa taarifa ndani ya klabu hiyo amesema baada ya kurejea nchini mwao, Mpanzu aliwasiliana na viongozi wa Simba ambao walionekana kutomhitaji tena, lakini kutokana na wanavyoiona timu yao, wanadhani wanahitaji winga wa aina yake.

"Mpanzu alikuwa akiihitaji sana Simba na alikuwa akipiga simu kwa viongozi kuwa sasa yupo tayari, lakini walimtolea nje, baadaye ikaonekana bado kikosi kina mapungufu hasa upande wa pembeni, kwa hiyo mazungumzo yakaanza tena, lengo ni kumsajili ili atusaidie tukishaingia hatua ya makundi," alisema mtoa taarifa huyo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, akikiri kuwa Mpanzu yupo nchini, lakini hakuwa tayari kusema kama ameletwa na timu hiyo.

"Sipapata mrejesho kutoka kwa mabosi wangu kam amekuja Simba au kwenye michakato yake, ila wote tunatambua dirisha la usajili limefungwa, litafunguliwa mwezi Desemba, ila ni jambo zuri kumpata mchezaji aina ya Mpanzu ili kuboresha maeneo yetu ya pembeni kulia na kushoto, waliopo waongeze juhudi zao, lakini kama kuongeza mtu mwingine kwa ajili ya kulifanya eneo hilo liwe hatari zaidi.

Ukiangalia kwenye soka la kisasa mabao mengi yanapatikana kutoka pembeni, ukiwa na watu makatili eneo la mawinga, unakuwa na mategemeo ya kupata mabao muda wowote ule," alisema Ahmed.

Taarifa zinasema kuwa bado wachezaji kama Joshue Mutale, Edwin Balua, Kibu Denis, bado hawajamshawishi kocha Fadlu Davids, akiwataka waongeze juhudi, lakini pia akiwaambia mabosi kuwa kama wanaweza kuongeza winga ambaye ana uwezo wa kupachika mabao wafanye hivyo.