Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unashiriki Maonesho ya Miaka 20 ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma na Biafra jijini Dar es Salaam, ili kuwahudumia na kutoka elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachama wake na wanachama watarajiwa (Wanafunzi wa elimu ya Juu).
Akizungumza kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Afisa Kumbukumbu za Wanachama Mwandamizi wa PSSSF Magira Werema, amesema, Maonesho hayo ni fursa nzuri kwa Mfuko kutoa elimu ya matumizi ya huduma mtandao (PSSSF Kidijitali). "Ifahamike kuwa PSSSF imefanya mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma sasa tumeachana na mfumo wa kuwahudumia wanachama wetu kupitia makaratasi, huduma zote zinatolewa kupitia mtandao, maarufu PSSSF Kidijitali," amesema.
Kupitia PSSSF Kidijitali, mwanachama anaweza kupata taarifa za michango yake, kufuatialia mafao, kujisajili, kuwasilisha madai mbalimbali na kwa wastaafu wanaweza kujihakiki kupitia simu janja.
Naye Afisa Mwandamizi wa Matekelezo PSSSF, Zainab Ndullah akizungumza kutoka viwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam, amesema wanachama wanaotembelea kwenye mabanda ya Mfuko watapata fursa ya kuelezwa kuhusu utekelezaji wa maagizo ya serikali ya kuanza kulipa Mafao kwa kutumia utaratibu wa kikokotoo kilichoboreshwa na tayari kuanzia Januari mwaka huu wa 2025 utekelezaji umeanza kwa ongezeko la asilimia 2 katika pensheni ya kila mstaafu na kima cha chini cha mstaafu kutoka 100,000 kwenda 150,000.
Pia katika maboresho hayo, mstaafu yeyote anayepokea pensheni katika Mfuko wa PSSSF akifariki, Mfuko utatoa kiasi cha Sh 500,000.00 kwa ajili ya maziko (funeral grant), huku Mstaafu yoyote akifariki wategemezi wake wanaotambuliwa na sheria ya Mfuko watalipwa mkupuo wa miezi 36 wa pensheni ya mwezi ya mwanachama husika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED