MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ameitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya Jiji la Arusha, huku akitaka kujua sababu za kuchelewa kumpata mkandarasi licha ya ahadi zilizotolewa mara kadhaa bungeni.
Akizungumza leo Februari 11, 2025, bungeni jijini Dodoma, Gambo amesema kuwa ameuliza swali hilo mara tatu bungeni na kila mara serikali imekuwa ikitoa majibu yanayokinzana.
“Tangu nimekuwa mbunge, nimeuliza maswali mara tatu kuhusu ujenzi wa stendi ya Jiji la Arusha, lakini majibu tunayopata hayaridhishi. Mara ya mwisho, Oktoba 31, 2024, serikali ilisema kuwa mkandarasi angepatikana na ujenzi ungeanza Januari mwaka huu. Leo hii tupo Februari, lakini hakuna chochote kilichofanyika,” amesema Gambo.
Ameendelea kunukuu majibu ya serikali yaliyotolewa awali bungeni, ambayo kwa mara ya mwisho yalieleza kuwa mpango wa ujenzi ulikuwa ukamilike kupitia mfumo wa NeST, na zabuni ilitangazwa Januari 19, 2024, huku tathmini ya mradi ikikamilika Julai 2024 na mkataba ukitarajiwa kusainiwa kati ya Novemba na Desemba 2024.
“Sasa Desemba 23 imepita, Januari 2025 imepita, leo tupo Februari. Ukienda Arusha eneo la Bondeni City, ardhi ipo, ekari 30, hati ipo. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kutuletea mradi wa TACTIC ili stendi ijengwe pale, lakini kwanini wataalamu wa manunuzi wanachelewesha kumpata mkandarasi? Serikali ituambie, tatizo ni nini?" amehoji Gambo.
Mbunge huyo pia amemtaja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, akisema hana shaka na usimamizi wake, lakini alitaka kujua ni kwa nini zabuni katika halmashauri nyingine zimefanikiwa kutekelezwa wakati Arusha bado inasuasua.
“Ni aibu kwa Arusha, jiji la kimataifa, kutokuwa na stendi ya kisasa. Rais amefanya kazi kubwa, Filamu ya The Royal Tour imeongeza utalii, mikutano inaendelea, mji umechangamka, lakini hatuna stendi ya kisasa. Serikali ituambie, kati ya haya majibu matatu waliotupa bungeni, lipi ni jibu sahihi ili nilipeleke kwa wananchi wa Arusha Mjini?,” amesema Gambo kwa msisitizo.
Akitoa majibu ya suala hilo, Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema kulikuwa na changamoto ndogo ndani ya serikali hata hivyo miradi yote iliyo chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC) unaofadhiliwa na serikali kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia wa thamani ya zaidi Sh. Trilioni 1.18 inaendelea.
Pia ameahidi kuwa wakandarasi wote wataanza kupata fedha za ujenzi wa miradi hiyo kuanzia wiki ijayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED