Kikwete ataja manne wasichana kuishi na sayansi

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:21 PM Feb 11 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira,Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira,Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira,Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ametaja mambo manne yanayopaswa kufanywa ili kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi ikiwamo kuanzisha utoaji motisha na kuendesha programu kabambe baina ya sekta za umma na sekta binafsi.

Kikwete aliyasema hayo leo, kwenye maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Wanawake na Wasichana katika Sanyasi yanayofanyika jijini Dodoma.

Alisema hatua hizo zinalenga kuleta mapinduzi katika ushiriki na mchango wa wanawake na wasichana katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) na utoaji motisha ufanyike kwa wanaoshiriki na kufanya vizuri katika STEM, utafiti na ubunifu nchini.

Waziri huyo alisema ni muhimu kuendelea kubuni njia na mikakati ya kuimarisha, kuratibu na ufugamanishaji mipango, programu na juhudi nyingine zinazolenga kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati na nyanja nyingine za kisayansi.

“Zifanyike tafiti mahsusi zinazolenga kubainisha hali halisi ya idadi ya wanawake na wasichana wanaojiunga na stem katika ngazi mbalimbali za elimu nchini katika kipindi kizichozidi miaka 10,”alisema.

 Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, anaeshughulikia Elimu Msingi, Dk. Charles Mahera alisema serikali itaendelea   kuandaa walimu wazuri wa masomo ya sayansi kwa lengo la kuwasaidia  wanawake na wasichana wapende kusoma masomo ya sayansi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  anaeshughulikia vyuo vikuu,Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi alisema maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha na kuongeza ushiriki wa wanawake na Wasichana katika nyanja za sayansi, uhandisi na hisabati ili wataalamu wawe wengi katika siku za mbeleni.