Kamati yabaini upungufu mkubwa walimu wa amali

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 04:59 PM Feb 11 2025
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko.

KAMATI ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imebaini kuwapo na uhaba mkubwa wa walimu wa amali wenye sifa na weledi ambapo mahitaji ni walimu 620 huku waliopo ni 62.

Kutokana na upungufu huo, Bunge limeezimia serikali iongeze bajeti ya kutosha ya kuajiri walimu wenye sifa na weledi wa masomo ya amali kulingana na mahitaji

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko ameyasema hayo leo bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo.

Amesema kuna upungufu wa walimu 558 pamoja na uhaba wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia na ukosefu wa miundombinu sahihi kama vile maabara na warsha za vitendo.

“Hali hii inakwamisha na kuzorotesha elimu ya amali nchini pamoja na utekelezaji wa mtaala wa mafunzo ya amali katika shule za Serikali, kwa hiyo Bunge linaazimia serikali iiajiri walimu na iwezeshe upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia katika shule za amali,”amesema

Pia, amesema  iboreshe vifaa na miundombinu muhimu katika shule za serikali ambazo zimeanza utekelezaji wa Mtaala katika Mkondo wa Amali, iweke mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kuandaa walimu wa masomo ya amali ili kuwawezesha wahitimu wa mafunzo hayo kusoma kozi hizo na kuajiriwa kama walimu na ipange vyuo maalumu kwa ajili ya mafunzo ya ualimu wa amali.