Kundi la wanamgambo wa M23 wanaotajwa kuungwa mkono na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) yamefanya mashambulizi tena baada ya kuwa kimya kwa siku kadhaa huku wakioneka kushambulia uelekeo wa barabara kuu ya Bukavu ili kukata njia za ugavi za jeshi la Kongo FARDC.
Mapigano hayo yanaibuka tena siku kadhaa mara baada ya viongozi wa Afrika Mashariki na Kusini kutoa wito wa usitishwaji wa mapigano hayo huku wakipendekeza mazungumzo bila masharti.
Kundi hilo ambalo mara kadhaa limenukuliwa likidai kutaka kuikomboa Kongo yote na kumwondoa madarakani Rais Felix Tshisekedi, limeendeleza mapigano yake karibu na kijiji cha Ihusi kilomita 70 kutoka mji Mkuu wa Jimbo la Bukavu na kilomita 40 kutoka uwanja wa ndege wa jimbo hilo, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama.
Shirika la habari la AFP limenukuu vyombo vya usalama vya ndani kuwa imesikika milipuko ya silaha nzito karibu na Uwanja wa ndege wa Kavumba unaotumiwa na jeshi la Kongo kusafirisha vifaa hadi eneo hilo na kambi yake kuu ya kijeshi.
Mpango huo ni sehemu ya kuhakikisha wanajeshi wa FARDC wanakosa huduma za kijeshi na kujiondoa wenyewe katika eneo hilo.
Kundi la M23 katika miezi ya hivi karibuni limekamata kwa haraka sehemu za eneo la mashariki mwa DRC lenye utajiri wa madini baada ya kuchukua tena silaha mwishoni mwa 2021, katika nchi iliyokumbwa na migogoro mingi kwa miongo kadhaa.
M23 ilianza kusonga mbele katika Kivu Kusini baada ya kuchukua udhibiti wa Goma, mji mkuu wa jimbo jirani la Kivu Kaskazini ambalo linapakana na Rwanda.
Bukavu imekuwa ikijiandaa kwa shambulio la M23 kwa siku kadhaa, huku shule zikifungwa katika jiji hilo siku ya Ijumaa ambako wakaazi wameanza kukimbia na maduka kufungwa kwa hofu ya kutokea shambulio hilo kubwa.
Februari 11, 2024 Benki zilionekana kufungwa jijini humo. Kutekwa kwa Bukavu kungetoa udhibiti kamili wa Ziwa Kivu.
Hata hivyo wanajeshi wa Burundi, ambao wanadaiwa kuonekana mashariki mwa DRC kuunga mkono jeshi la Kongo, walisimamisha kwa muda harakati za M23.
Takriban wanajeshi 10,000 wa Burundi wametumwa Kivu Kusini, Bujumbura ilituma kikosi kimoja cha ziada katika eneo hilo Ijumaa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED