Pinda aonya maofisa ardhi wanaokiuka maadili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:14 AM Sep 21 2024
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda
Picha: Mtandao
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amesema hakuna ofisa ardhi atakayehamishwa eneo la kazi endapo akikiuka maadili ya utendaji wa taaluma yake.

Alitoa onyo hilo juzi wakati mkutano wa pamoja wa wananchi na watumishi wa ardhi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa Kilimanjaro.

"Nikimwambia Katibu Mkuu huyu utendaji kazi wake unaripotiwa kwamba hafai, tutatuma vyombo vitakuja kukutafakari upya.

"Usikubali dawati lako liwe chanzo cha mgogoro, upelekwe kwa Mkuu wa Wilaya, kwa Mkurugenzi, kwa mbunge na jamno lile uliloanzisha wewe linakwenda mpaka kwa Rais. Haiwezekani! Kila mtu ajitafakari," alionya Pinda.

Naibu Waziri huyo pia alitoa maelekezo kwa Ofisi za Wasajili wa Hati nchini kuharakakisha mchakato wa utoaji hatimiliki za ardhi ili wananchi waweze kunufaika nazo ikiwa pamoja na kuaminiwa kupata mikopo katika taasisi za kifedha.

"Maelekezo ninayoyatoa kwenye dawati la usajili usilaze kazi, toeni hati ziende kwa wananchi," aliagiza Naibu Waziri Pinda. 

Kiongozi huyo pia aliwaonya maofisa ardhi wanaojiuhusisha na ugawaji kiwanja kimoja mara mbili na kusisitiza kuwa wizara yake itachukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya mtumishi yeyote atakayekiuka maadili ya utumishi wa umma kwa taaluma yake.

"Kama litamhusisha ofisa wa kwetu kwenye jambo la kugawa kiwanja kimoja mara mbili, sasa hivi hatunamswalia Mtume, tutachukua hatua kali," alionya.

Naibu Waziri Pinda alihitimisha ziara yake mkoani Kilimanjaro jana, ambako mbali mambo mengine, alisikiliza na kutatua changamoto za ardhi kwa wananchi wa mkoa huo pamoja na kufanya vikao kazi na watumishi wa ardhi mkoani humo.