LATRA yarejesha barabarani mabasi sita ya Katarama

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 07:22 AM Sep 21 2024
Kampuni ya Katarama.
Picha: Mtandao
Kampuni ya Katarama.

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeruhusu mabasi sita kati ya 10 ya kampuni ya Katarama kuanza kufanya kazi.

Wiki iliyopita LATRA ilisitisha kwa muda usiojulikana leseni ya utoaji huduma kwa mabasi yote ya kampuni hiyo kuanzia Septemba 13 mwaka huu kutokana na ukiukaji sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji, ikiwamo kuchezea mifumo ya udhibiti wa mwendokasi.

Baada ya kusitisha huduma kwa mabasi ya kampuni hiyo, LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walianza kufanya uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa LATRA, Salum Pazzy, alisema kuwa baada ya kufanyika uchunguzi wa awali, wamebaini kwamba kati ya mabasi 10, manne ndio yalibainika kuchezea mfumo.

"LATRA pamoja na kudhibiti, kisheria pia imepewa mamlaka ya kuwalea wasafirishaji kuhakikisha biashara yao inalindwa na wakaendelea kustawi kwa ajili ya kutoa huduma. Kuliko kuendelea kusimamisha mabasi yote, iliona bora itoe rukhsa hayo sita ambayo hayakufanya makosa.

"Lakini kabla ya hapo, iliita uongozi wa mabasi hayo kuwapatia masharti kabla ya kuwaruhu na wakaahidi kutekeleza, hivyo tunaamini kwamba wakati haya mengine manne yanayoendelea kuchunguzwa, hayo yaliyoruhusiwa yatafanya vizuri kwa sababu kama mamlaka hatuko tayari kuona maisha ya Watanzania wanaotumia huduma yao yanakuwa hatarini," alisema.

Baadhi ya makosa ambayo yalibainika kufanywa na mabasi hayo ni pamoja na kuondoa kifaa kilichofungwa na LATRA katika mabasi na kufanya ujanja wa kufunga kifaa chao kingine cha kutuma taarifa zisizo sahihi kwa Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS). 

"Pia yalibainika kufanya vurugu barabarani kwa mwendo kasi na kung’oa sehemu ya kifaa kinachotuma taarifa ya mwenendo wa mabasi na kubadilisha kifaa cha antena na hivyo kutuma taarifa zisizo sahihi kwa mamlaka," alisema.

Pazzy alisema mamlaka inaendelea kufuatilia mabasi yote yanayovunja sheria na haitosita kuchukua hatua kwa wasafirishaji wote wanaokiuka sheria na taratibu za usafirishaji.