Atiwa mbaroni kwa tuhuma za kumtoboa macho mtalaka wake

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:41 AM Sep 21 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Paulo Shija (19), mkazi wa Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za kumjeruhi na kumtoboa macho yote mtalaka wake, Ester Mataranga (25), mkazi wa Ndala.

Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi alisema walipokea taarifa ya tukio hilo Agosti 13 mwaka huu kuwa Shija alimtoboa macho yote mawili kisha kutokomea kusikojulikana.

"Baada ya kupokea taarifa hiyo, tulifika eneo la tukio na kumchukua majeruhi huyo na kumpeleka katika Hospitali ya Kolandoto iliyoko Halmashauri ya Kishapu kwa ajili ya kupewa matibabu," alisema SACP Magomi.

Alisema kuwa baada ya hatua hiyo, jeshi hilo liliendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na wananchi na kufanikiwa kumtia mbaroni Septemba 17 mwaka huu.

"Tulimkamata akiwa maeneo ya Masekelo, Manispaa ya Shinyanga na kumfikisha kituoni kwa taratibu zaidi za kisheria na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani. Tunakemea vikali wananchi wote wanaojichukulia sheria mkononi," alisema Kamanda.

Akizungumza na Nipashe hospitalini hivi karibuni, Ester (25) alidai kutobolewa macho na mtalaka wake huyo (Shija), wakati wakielekea kwenye nyumba walikokuwa wanaishi awali kwenda kuchukua mizigo yake na talaka iliyokuwa imeandaliwa baada ya mtalaka wake kuoa mwanamke mwingine.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 13 mwaka huu saa 12 asubuhi na kuwa awali walikuwa wanaishi vyema katika ndoa yao na walibahatika kupata watoto wawili, lakini baadaye walikorofishana kutokana na kile alichodai "wivu wa mapenzi".

Alidai kuwa mtalaka wake huyo alikuwa akimtuhumu kutoka nje ya ndoa na kulazimika kurejea nyumbani kwao katika Kijiji cha Kundikiria-Ukeme na kuendelea na maisha mengine pamoja na wazazi wake.

Ester alidai kuwa akiwa nyumbani kwa wazazi wake, walikuwa wakiwasiliana mara kwa mara na Shija kumwomba arejee Ndala walikokuwa wanaishi kwenda kuchukua mizigo yake baada ya mtalaka wake huyo kuoa mwanamke mwingine.

"Nilianza safari Agosti 10 kwenda kuchukua mizigo na talaka pia. Siku ya Jumapili ya tarehe 11 Agosti, nilimpigia simu mtalaka wangu na kumwambia ningefika Ndala tarehe 12 Agosti mwaka huu na tulikubaliana na nilipofika Kituo cha Mabasi Shinyanga (Manyoni), alinipokea vyema.

"Nilipatiwa chakula na kupelekwa nyumba ya kulala wageni kwa ajili ya kupumzika kusubiria siku iliyokuwa inafuata tuelekee nyumbani," alidai.

Ester anaendelea kusimulia kuwa siku hiyo walilala pamoja na ilipotimu saa 10 alfajiri ya tarehe 13 Agosti, mtalaka wake huyo alimlazimisha waondoke lakini alikataa kwa maelezo kuwa aliona ilikuwa usiku sana na ilipotimu saa 12 asubuhi walitoka na kungozana pamoja.

"Tulipofika sehemu ya kichaka, barabara ya Musoma Food, mtalaka wangu alidai anataka kujisaidia haja ndogo. Mimi nikatangulia mbele, ghafla nikakabwa.

"Alinivuta kwa nguvu kanga niliyokuwa nimejitanda shingoni. Nikaanza kukimbia huku nikipiga kelele kuomba msaada.

"Baada ya kuona viashiria vibaya, alinikaba shingo na kuishiwa nguvu na kuanguka chini na alijua ameniua na kunitoa macho. Nimekuja kushtuka niko hospitalini nikipatiwa matibabu," alidai Ester.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto aliyempokea mgonjwa na kuanza kumpatia matibabu, Dk. Wallace Sahani alisema Ester ametobolewa macho yote, lakini jicho moja limeharibika kabisa na lingine linahitaji matibabu ya kibingwa na wanatarajia kumpatia rufani apelekwe katika Hospitali ya Kanda ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.

"Jicho lake moja halioni vizuri, kuna damu imevujia ndani, hivyo talazimika kumpatia rufani akapate matibabu ya kibingwa ili aweze kuona vizuri, kwani alifika akiwa na hali mbaya akiwa na majeraha makubwa lakini kwa sasa tumeyaweka sawa," alisema Dk. Sahani.

*Imeandaliwa na Vitus Audax na Shaban Njia