Dk.Gwajima: Ustawi wa jamii kuwa idara kamili inayojitegemea

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:45 AM Sep 21 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum  Dk. Dorothy Gwajima
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima

Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii inayojitegemea chini ya Wizara yenye dhamana ya masuala ya Ustawi wa Jamii ili kurahisisha na kuimarisha uratibu, usimamizi na utekelezaji wa afua za Ustawi wa Jamii nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum  Dk. Dorothy Gwajima leo wakati akifunga Mkutano wa tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Waziri Dk. Gwajima amesema lengo la kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii itakayojitegemea ni ongezeko la uhitaji wa huduma za Ustawi wa Jamii kisekta kunakohitaji Taasisi madhubuti katika kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma hizo katika jamii kupitia Taasisi za umma, binafsi na wananchi kwa ujumla.

Amebainisha kwamba, hatua hiyo ni matokeo ya kukubaliwa kwa  wasilisho la mapendekezo ya Haki Jinai kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo mpango huo kwa sasa unasubiri maelekezo ya muundo wa Idara hiyo kupitia Wizara ya Utumishi.