Wawili wauawa kisha miili yao kuchomwa moto tuhuma wizi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:11 AM Sep 21 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe

WATU wawili wakazi wa Mtaa wa Buzunza, mkoani Simiyu, wanadaiwa kupigwa hadi kufariki dunia kisha miili yao kuteketezwa kwa moto wakituhumiwa kukutwa na mali zinazodhaniwa za wizi.

Wawili hao ni Ntawa Limbu (32) ambaye ni mkulima pamoja na mwenzake aliyetambulika kwa jina moja la Suma, wote ni wakazi wa Mtaa wa Buzunza, mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji hayo.

Alisema watu hao wanatuhumiwa kujichukulia sheria mkononi kwa kuwakamata na kuwaua watu wawili kisha kuteketeza miili yao kwa moto.

"Chanzo cha kufanya uhalifu huo wa kujichukulia sheria mkononi ni kwamba, inasemekana wawili hao walikuwa wanamiliki mali zinazosadikika kuwa za wizi na mara baada ya taarifa kumfikia aliyewahi kuibiwa, alihamasisha kundi la vijana waendesha bodaboda na kuanza kuwatafuta watuhumiwa ambao kwa sasa ni marehemu," alisema.

Kamanda Edith alisema Jeshi la Polisi linakamilisha uchunguzi ili taratibu zingine za kisheria zifuate ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.

"Tunaendelea kutoa wito kwa wananchi kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi kwani ni kosa kisheria, Jeshi la Polisi litawakamata na kuwafikisha mahakamani," alisema Kamanda Edith.