21 wakamatwa kwa tuhuma za mauaji

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 07:25 AM Sep 21 2024
21 wakamatwa kwa tuhuma za mauaji
Picha:Mtandao
21 wakamatwa kwa tuhuma za mauaji

JESHI la Polisi Mkoa wa Singida linawashikilia watu 21 kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya mauaji.

Kati yao, 13 wameunganishwa katika kesi ya mauaji inayomkabili mganga wa kienyeji aliyetuhumiwa kuua watu 10 na kuwazika katika makazi yake.

Mganga huyo, Kamba Kasubi, anadaiwa kuua watu hao na kuwazika katika makazi yake kijijini Makuro, wilayani Singida na katika Kijiji cha Porobanguma, wilayani Nchemba, mkoani Dodoma kwa nyakati tofauti.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Mayunga Mayunga, akizungumza na waandishi wa habari juzi mjini hapa, alisema kuwa katika kipindi cha Julai hadi Agosti mwaka huu, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 137 wa makosa mbalimbali katika doria na misako ya kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu.

"Watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya kutenda makosa tofauti yakiwamo makosa ya mauaji (watuhumiwa 21), watuhumiwa 34 kwa kukutwa na pikipiki zinazodhaniwa kuwa ni za wizi na watuhumiwa 21 wa dawa za kulevya aina ya bangi gramu 8,773," alisema.

Kaimu Kamanda Mayunga alisema watuhumiwa wengine wanne walikamatwa na dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa gramu 19,842, mmoja akiwa dawa aina ya Heroin uzito wa gramu 0.5, wakati wengine 15 walikutwa na pombe haramu ya moshi lita 78.

Aliongeza kuwa watuhumiwa watano walikamatwa kwa makosa ya kubaka, watatu kwa tuhuma za wizi wa kompyuta, watano kwa tuhuma za wizi wa simu ndogo, wanne kwa tuhuma za wizi wa mitungi midogo ya gesi, mmoja kwa wizi wa TV mbili na wengine walikamatwa kwa tuhuma za wizi wa redio, mifugo huku watatu wakidaiwa kukutwa na nyara za serikali.

"Jeshi la Polisi linawashukru wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kubaini na kuzuia uhalifu na linawaomba kufika mahakamani kutoa ushahidi ili kesi za mauaji hayo ziweze kupata mafanikio," alisema.