Arejeshewa tabasamu baada ya kuondolewa uvimbe wa kilo tano

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:54 AM Sep 21 2024
Arejeshewa tabasamu baada ya  kuondolewa uvimbe wa kilo tano
Picha:Mtandao
Arejeshewa tabasamu baada ya kuondolewa uvimbe wa kilo tano

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imemrejeshea tabasamu Kalume Kalume (41) baada ya kufanyiwa upasuaji rekebishi kwa kumwondoa uvimbe wa kilo tano uliomsumbua kwa zaidi ya miaka 25.

Kalume ambaye ni mkazi wa Lindi, alikuwa anasumbuliwa na uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake, Baada ya upasuaji huo, ameruhusiwa kwenda nyumbani.

Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Rekebishi na Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Rekebishi, Dk. Laurean Rwanyuma, aliongoza jopo la wataalamu wenzake kumfanyia upasuaji uliodumu kwa saa nne.

Alitoa ufafanuzi huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upasuaji huo, akisema kuwa baada ya uchunguzi wa kina kukamilika, iligundulika kuwa Karume alikuwa na uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake hasa shingoni, begani na kifuani na ugonjwa huo kitaalam unaitwa 'Plexiform Neurofibromatosis'.

Alisema matibabu ya ugonjwa huo ni kuondolewa kwa njia ya upasuaji. Agosti 30 mwaka huu walimfanyia.

Dk. Rwanyuma alisema ugonjwa aliopata Kalume si wa kuambukiza, bali ni wa kuzaliwa nao, akiurithi kutoka kwa wazazi wake au mzazi mmoja.

Alisema ugonjwa huo hushambulia mishipa ya fahamu na kujitokeza kwa njia mbalimbali.

Dk. Rwanyuma alisema mtu anapata ugonjwa huo kutokana na kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi na si kila mtoto anaweza kuwa navyo.

Alisema matibabu yake kama uvimbe utakuwa mkubwa, ni kukata na upo uwezekano wa uvimbe huo kurejea tena.

"Unaweza kurejea baada muda kama miaka mitano. Mtu anaweza kupata uvimbe ambao ni mkubwa sana, unakuwa mzigo kwake. 

"Wapo wanaopata usoni, unaondoa mwonekano, hivyo unaondolewa ili kumwezesha kufanya shughuli zake za kila siku. Wagonjwa wa namna hii ambao tunawapokea hospitalini hapa kwa mwezi huwa hadi watano," alisema.

Mtaalamu huyo pia alisema wapo wanaorithi vinasaba vya ugonjwa huo, lakini uvimbe ukawa mdogo.

"Kama umemwona mama yake Kalume, yeye anavyo vidogovidogo ambavyo havihitaji upasuaji. 

"Wito wetu; mtoto anapozaliwa basi aangaliwe kama ana alama yoyote. Dalili za ugonjwa huu unakuta mtoto ana baka mwilini.

"Huwa na rangi kama chai ya maziwa iliyowekwa kahawa, ukiona hivyo, fika kwa wataalamu ili kubaini kama ni ugonjwa huu," alielekeza.

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk. Rachel Mhaville, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, alisema mara baada ya kumpokea mgonjwa huyo mwezi uliopita, hospitali ilifanya jitihada za dhati kuhakikisha anaonwa na madaktari bingwa na kufanyiwa vipimo mbalimbali.

"Tunawapongeza waandishi wa habari kwa kumwibua mgonjwa huyu na kumleta hospitalini, kwani ndipo penye madaktari bingwa bobezi wa upasuaji rekebishi walioweza kumpa huduma stahiki na kumrejeshea mwonekano unaompa faraja na tabasamu," alisema Dk. Mhaville.

Aliwaomba wasamaria wema kuendelea kujitokeza kuchangia huduma kwa watu wasiokuwa na uwezo, akiwamo Karume ili kukamilisha malipo ya huduma alizopata kupitia namba ya malipo 994501766575 yenye jina Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mjomba wa Kalume, Salum Idobelele, alisema alihangaika na Karume tangu akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kupata uvimbe huo.

"Mwaka huu ndipo alipokutana na waandishi wa habari kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam ambao walibeba jukumu la kumtafutia msaada wa matibabu kwa kumpeleka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Temeke na kisha kupewa rufani kwenda Muhimbili.