Naibu Waziri Mkuu atoa maagizo matano ufuatiliaji na tathmini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:02 AM Sep 21 2024
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
Picha:Mtandao
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amezitaka taasisi za ufuatiliaji na tathmini kufanya kazi kwa weledi na kuimarisha eneo hilo ili kuendana na mahitaji yanayolenga kuleta tija katika utoaji huduma kwa wananchi.

Alielekeza hayo jana Zanzibar wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Kongamano la Tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza.

Dk. Biteko alisema wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini wanawajibika kulinda taaluma hiyo na kuwashawishi kwa hoja wakuu wa taasisi husika kupenda kazi zinazotokana na taaluma hiyo badala ya kujisikia wanyonge kitaaluma.

Naibu Waziri Mkuu Biteko aliwataka washiriki muda wote kusisitiza misingi ya taaluma hiyo na baadaye kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa na watu wake. 

"Inawezekana katika maeneo yenu ya kazi wakawapo wakuu wa taasisi au viongozi wa serikali ambao hawapendi mfanye kazi yenu vizuri, kukubaliana na hilo ni kujiua wenyewe.

"Mnapotoka hapa mkafanye mkuu wa taasisi au kiongozi aone umuhimu wenu katika shirika," aliagiza Naibu Waziri Mkuu Biteko.

Aliwataka wataalamu hao kusema ukweli na kusimamia taaluma yao, akisema "Ninataka niwaombe mkajiamini, Rais Samia ameagiza na kuelekeza kuwapo vitengo vya tathmini ndani ya serikali.

"Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wafanye kazi na kitengo cha ufuatiliaji kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu, mfuatilie fedha zinazopelekwa kwenye miradi na matokeo yake kwenye kubadilisha hali za maisha ya watu," alisisitiza Dk. Biteko.

Kupitia kikao hicho, Naibu Waziri Mkuu alitoa maagizo matano yakilenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na kujifunza.

"Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu ikamilishe mapema Mfumo Ufuatiliaji na Tathmini na kuwezesha taarifa za utendaji wa Serikali kupatikana kwa urahisi.

"Tume zetu za Mipango zikamilishe uchambuzi wa miradi yote inayotekelezwa ndani ya serikali na kila mwaka kutoa taarifa ya utekelezaji. Namna hii itawezesha serikali kuona tija ya miradi inayoidhinishwa na kutekelezwa nchini," aliagiza.

Dk. Biteko alielekeza ofisi hiyo kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili iwezeshe utekelezaji sahihi wa eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini. 

Aliagiza TanEA na ZaMEA kuwa sera pamoja na mikakati yake viwe zinafanyiwa tathimini kila baada ya miaka mitatu baada ya kuandaliwa. 

"Hii itasaidia kujua kila hatua inayofikiwa kwa utelezaji wake pamoja na utatuzi wa changamoto za utelezaji na maboresho wakati wa uhuishaji sera," aliagiza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi alisema Kongamano hilo la tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau na washiriki. 

Alitaja lengo la kongamano hilo kuwa ni kuweka  msisitizo kwenye lengo kuu la serikali la kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi na kuwa katika kutimiza azma hiyo, washiriki wakihamasishwa kutumia vizuri taaluma na mafunzo mbalimbali wanayoyapata kuhakikisha wanakuwa jicho la serikali katika mipango yake, utendaji wake na utekelezaji miradi.

Lukuvi alisema Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais Hussein Ali Mwinyi wamekuwa vinara wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji wa serikali kwa ujumla wake, utekelezaji wa miradi yote nchini na utoaji huduma bora kwa wakati kwa wananchi wote. 

Alisema kuwa marais hao wanafanya hayo ikiwa ni utekelezaji Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambapo kwa sekta zote umewekwa mkazo wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji, utekelezaji miradi na utoaji huduma.

"Katika kuimarisha Sekta ya Fedha, ibara ya 20(f) ya Ilani ya CCM inaitaka serikali kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya mashirika na taasisi zilizobinafsishwa ili kuhakikisha mikataba inatekelezwa ipasavyo na sekta ya ujenzi, ibara ya 51(a)(ii) ya Ilani inaitaka serikali kuboresha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za barabara kwa kuhakikisha thamani ya ubora wa kazi inaendana na fedha zilizotumika," alisema Lukuvi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk. Jim Yonazi alisema kuwa kupitia kongamano hilo wamepata fursa mbalimbali ikiwamo kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa wataalamu. 

Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Dk. Ameir Haji Sheha alisema kongamano hilo limejumuisha washiriki 738, akishukuru Ofisi ya Waziri, Sera, Bunge na Uratibu kwa ushirikiano wakati wote wa maandalizi wa kongamano hilo.