ACT yadai kunusa harufu ya rushwa mabaraza ya ardhi

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:07 AM Sep 21 2024
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu
Picha:Mtandao
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amekemea kile alichokiita "rushwa kwa baadhi ya viongozi katika mabaraza ya ardhi", akidai hali hiyo inachangia kuwapo migogoro ya kudumu.

Dorothy alitoa kauli hiyo juzi wilayani Kiteto, mkoani Manyara, akiwa katika mwendelezo wa ziara zinazofanywa na viongozi wakuu wa chama hicho waliojigawa kikanda.

Alisema Kiteto ni "ni moja ya makao makuu ya migogoro ya ardhi" ambayo inasababishwa na mgongano kati ya wakulima na wafugaji.

Alisema changamoto hiyo si ya Kiteto peke yake, bali iko katika maeneo mengi, ikihusisha wakulima na wafugaji, wakulima na wananchi, serikali na wananchi, mwekezaji na mwananchi.

"Kasi ya serikali haioneshi kwamba migogoro itakwisha, tulitegemea serikali ingejipanga vizuri na kuongeza kasi kushughulikia matatizo hayo.

"Kama taifa bado hatuna mifumo bora ya kutatua changamoto za ardhi na hata wanaoongoza mabaraza ya ardhi, hawajapewa elimu ya kutosha ya namna ya kuitatua," alisema Dorothy.

Alisema chama chao kitakapoingia madarakani, kitahakikisha kinawashirikisha wananchi kikamilifu kupanga matumizi ya ardhi, ili kuepukana na migogoro ya kila siku.

Alisema wangeweza kutenga ardhi kutokana na mahitaji husika na kuondoa migogoro yote, lakini kuna suala la rushwa katika mabaraza ya ardhi ambako wanatamani migogoro inavyopelekwa huko itatuliwe.

Dorothy aliwaambia wananchi wa Kiteto kwamba, migogoro hiyo isipochukuliwa kwa umuhimu wake, athari yake ni kubwa na inaweza hata kusababisha mauaji.

"Chama chetu kina sera itakayomaliza changamoto hii, mojawapo ni kuondoa ardhi mikononi mwa Rais. Tutawekeza katika mahakama inayotembea kutatua migogoro ya ardhi," alisema Dorothy. 

Kiongozi wa chama huyo pia aliwaomba wananchi wa Kiteto kuchagua viongozi wanaotokana na chama hicho ili waje na mbinu mbadala alizoziiita "za kukomboa nchi".

"Hatutakubali kilichotokea katika uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020 kitokee tena awamu hii. Ni wajibu wenu kuchagua kiongozi tunayemtaka, lakini tunafahamu namna ambavyo kumekuwa na vitisho kwa viongozi wa upinzani ili turudi nyuma," alidai Dorothy.

Kukiwa na madai hayo ya rushwa kwa baadhi ya watendaji wa ardhi, juzi Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, akiwa mkoani Kilimanjaro, alionya watendaji wa ardhi wanaokiuka maadili, akisisitiza hakuna afisa ardhi atakayehamishwa eneo la kazi endapo akikiuka maadili ya utendaji wa taaluma yake.