Ulega awataka wafugaji kufuata sheria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:45 AM Sep 21 2024
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega
Picha: Mtandao
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amewataka wafugaji kuishi kwa amani na kuheshimu sheria za nchi ikiwamo kuacha tabia ya kuingiza na kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

Waziri Ulega alisema hayo wakati wa kikao cha kusikiliza kero na changamoto za wafugaji wa Wilaya ya Namtumbo, kilichofanyika wilayani humo Septemba 19.

“Wafugaji muishi na watu vizuri, acheni ubabe, fuateni sheria, msiingize mifugo katika mashamba ya watu kwa makusudi, ni jambo baya sana, msipofuata sheria kila mtu mtamuona mbaya,” alisema.

Aidha, aliwataka wafugaji hao kuunda mabaraza ya wazee ya wafugaji ili yasaidie kusuluhisha migogoro na kukemea wachache wanaotaka kuharibu taswira ya ufugaji nchini.

Aliwahimiza wafugaji hao kuweka utaratibu wa kuvuna mifugo yao na kuiuza, kwa kuwa kutawasaidia kujipatia kipato na pia kupunguza wingi wa mifugo ili kujiepusha na migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amewaelekeza wataalamu kutoka wizarani kwake kwenda kutoa elimu ya ufugaji bora na fursa zilizopo kwenye ufugaji kwa viongozi, wafugaji na makundi mengine katika wilaya hiyo ili wajue umuhimu wa uchumi jumuishi.