WAZARAMO wana msemo wao, 'usinene ukamala', ukiwa na maana usiongee ukamaliza maneno kwani yanaweza kukurudia. Msemo huu una maana nyingi, ikiwemo kwamba unaweza kumsema na kumlaumu mtu, lakini kumbe ikawa sivyo ulivyodhani, au ikawa ni bahati mbaya tu. Mara nyingi ikija kudhihirika kwamba si kweli kwa jinsi ulivyomtuhumu unabaki na aibu.
Hili limeonekana Jumanne iliyopita, baada ya Taifa Stars kuwaumbua wahafidhina wote waliokuwa wameongea maneno mengi kuhusu timu hiyo.
Kuanzia mashabiki wa soka, mpaka baadhi ya wachambuzi walikuwa wameikatia tamaa Stars baada ya suluhu nyumbani dhidi ya Ethiopia, Septemba 4, ambapo kila mmoja hakutarajia kama ingeweza kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea.
Suluhu dhidi ya Ethiopia ilizua mengi sana. Wengine waliponda kikosi kilichopangwa na makocha Hemed Suleiman 'Morocco' na msaidizi wake, Juma Mgunda. Wapo waliosema Stars haishindi kwa sababu wachezaji wengi wa kikosi hicho hawapati namba kwenye timu zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wapo waliohoji hata kwa nini Stars ina makipa Ali Salim wa Simba na Abutwalib Mshery wa Yanga ambao kwenye vikosi vya timu zao siyo makipa namba moja.
Ushauri wao ukawa iletwe kanuni ya kuwaondoa makipa wote wa kigeni kwenye ligi na wadake wazawa tu. Yote hii ilikuwa ni hasira ya Stars kutopata ushindi.
Sasa wapo waliodhani kuwepo kwa wachezaji 12 wa kigeni kunawafanya wazawa wakose nafasi kwenye vikosi vyao na hii inasabisha Stars isiwe na kikosi cha wachezaji bora, hivyo wapunguzwe au waondolewe kabisa.
Bado wapo mashabiki wanaodhani kuwa Tanzania haina uchaguzi sahihi ya wachezaji bora, ndiyo maana inaonekaa kama haina wachezaji wenye viwango.
Mambo yalikuwa mengi sana, wengine walianza kuorodhesha hata wachezaji wa Kitanzania waliopo nje ya nchi nao waitwe ili waokoe jahazi la Stars, wengine wakaishauri Serikali kukubali uraia pacha ili Tanzania iwe na wachezaji wenye uraia wa nchi mbili kwani wapo wachezaji wa aina hiyo na ni wengi huko nje ya nchi.
Presha ilikuwa kubwa sana. Kuanzia kwa mashabiki, wachambuzi, makocha na wachezaji wa Stars ikawa ni presha kila mahala.
Ikaonekana kama haitokuwa na uwezo wa kufanya vyema, na hata mechi dhidi ya Guinea wengi waliikatia tamaa.
Baada ya kushinda kila mmoja sasa anameza maneno yake. Wote walioponda sasa wanasifu. Unaweza kudhani kama siyo wale waliokuwa wanaponda.
Hatusikii tena wachezaji wa kigeni wanazuia wazawa kwenye ligi, wala kupunguzwa na makipa kutoka nje ya nchi.
Hii inatufundisha mashabiki wa soka kuwa na subira kwa sababu soka ni mchezo wenye matokeo matatu, kushinda, sare na kupoteza. Na mpira unaweza kushinda popote pale.
Inatufundisha pia mashabiki wa soka na wachambuzi kufanya tathimini za kimpira na za kisayansi na si za kimihemko.
Kushinda Taifa Stars, kufungwa au sare, hakuhusinai na wingi au uchache wa wachezaji wa kigeni, badala yake ni matokeo tu ya mpira.
Haya Stars imeshinda, wachezaji 12 wa kigeni na kipa wao wameondoka? Ifike wakati mashabiki wa soka na wachambuzi wasiongee na kumaliza maneno ya sababu ya mihemko. Juzi tumeiponda Stars, leo imeshinda maneno yameturudia wenyewe, tunayakana, tunaisifia Stars.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED