ACT Wazalendo wameanza, vyama vingine vifuate

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:54 AM Sep 18 2024
 ACT Wazalendo,
Picha: Mtandao
ACT Wazalendo,

MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, amezawadiwa gari ya kutembelea na chama chake, ikiwa ni utekelezaji wa sera ya kuenzi viongozi wastaafu, kwa kutambua mchango wao kwa chama na taifa.

 Kwa mujibu wa viongozi wa ACT Wazalendo, sera hiyo inakusudia kuwaenzi viongozi wastaafu ambao wakati wa uongozi wao, walikitumikia chama kwa heshima, bidii , uaminifu na uadilifu mkubwa.
 
 ACT Wazalendo inawataja viongozi wanaohusika katika sera ya kuenziwa kuwa  ni kiongozi wa chama na  mwenyekiti wa chama wastaafu.
 
 Aidha,  chama kinasema, wanapata posho ya kila mwezi pamoja na huduma hiyo wanapatiwa bima ya afya ambayo aina yake  na posho ya kujikimu vitaamuliwa na Kamati ya Uongozi Taifa.
 
 Kadhalika, wana sharti kuwa viongozi hao wasiwe wamekihama au kufukuzwa chama, wakitumikie chama kwa heshima na utii, huku Kamati ya Uongozi Taifa ikiwa na jukumu la kuamua iwapo kiongozi husika alikitumikia chama kwa heshima na utii.
 
 Katika sera hiyo, chama kinasema, iwapo kiongozi atakuwa hana nyumba, chama kitamlipia pango la nyumba kwa kiwango ambacho kitaamuliwa na  kamati hiyo , lakini pia kuna sharti kuwa viongozi hao wasiwe wamekihama au kufukuzwa chama, tena wawe wamekitumikia chama kwa heshima na utii, huku Kamati ya Uongozi Taifa ikiwa na dhamana ya kuamua iwapo kiongozi alitimiza takwa hilo.
 Kwa utaratibu huo ACT Wazalendo, inastahili  kuigwa na vyama vingine vya siasa, kutambua mchango wa viongozi wastaafu wa vyama vyao kwa kuwapa zawadi kama kumbukumbu ya huduma yao kwao na umma pia.
 
 Huo ndio utaratibu wa sera ya chama hicho, ambao ninaamini unaweza kupunguza mtindo wa baadhi ya viongozi kuhama vyama vyao, badala yake watulie sehemu ili hatimaye wastaafu na kuenziwa.
 
 Kwa kuwa lengo la kuwaenzi viongozi wastaafu ni kulinda heshima yao,   kutambua mchango wao, kuendelea kunufaika na mawazo na fikra zao, katika ujenzi wa chama na kuwatunza na kuwahudumia kadri ya uwezo wa chama, utaratibu huo unafaa kuigwa hasa suala la afya.
 
 Labda nami ningeongezea kidogo kwamba pamoja na huduma ambazo chama hicho kimeorodhesha kwa ajili ya wastaafu wake, hili la huduma ya afya kwa wastaafu wake limenigusa.
 
 Ninaeleza hivyo, kwa sababu, moja ya vikwazo ambavyo wastaafu wengi wamekuwa wakikumbana navyo ni kukosa matibabu ya uhakika. Hicho ndicho kilio chao cha muda mrefu cha wazee na wastaafu.
 
 Katika huduma ambazo chama hicho kimezibainisha, kwa ajili ya wastaafu wake, tiba au bima ya matibabu  inaweza kuwa namba moja, hivyo kwa sera hiyo, vyama vingine vimepata cha kujifunza.
 
 Ninadhani chama hicho kimetambua kuwa bila afya bora, hata hayo mengine ambayo kimepanga kuwafanyia wastaafu wake, hayawezi kuwa na maana bila kuwa na afya imara.
 
 Huduma ya afya ni ya msingi kuliko huduma nyingine. Iwapo vyama vingine vitaamua kuiga baadhi ya vitu kutoka kwenye sera hiyo, basi vichukue hiyo huduma ya afya.
 
 Iwapo hilo litafanyika, linaweza kuwafanya wanasiasa kuwa na uhakika wa kuhudumiwa afya zao hata wakiwa nje ya ulingo wa siasa, kuliko kuwaacha tu huku wakiwa na mchango kwenye vyama.

Ikumbukwe kuwa utumishi wa watu ni jukumu lisilolipika kwa gharama yoyote kwa vile wapo viongozi wanaotoa maisha na mali zao kwa ajili ya uhai wa taasisi kama vyama vya siasa.

Mambo hayaishii hapo kuwatetea Watanzania wanyonge na kuibua shida zao ni jingine ambalo viongozi wa kisiasa wanalifanya.

Ni jambo jema kuwathamani na kuwaenzi wafia siasa na maendeleo ya demokrasi ikibidi waanzishiwe makumbusho ya wanasiasa na watetezi wa siasa za kukosoa na kushauri serikali.