Tusimalize maneno kwa Stars, tuendelee kuiunga mkono

Nipashe
Published at 07:19 AM Sep 14 2024
Wachezaji wa Timu ya Taifa.
Picha:Mtandao
Wachezaji wa Timu ya Taifa.

TIMU ya taifa ‘Taifa Stars’ bado ipo kwenye kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Afrika (AFCON) za mwaka 2025 zitakazofanyika nchini Morocco.

Tunasema Taifa Stars bado wapo kwenye kampeni za kusaka tiketi hiyo kwa sababu ya matokeo waliyoyapata kwenye mchezo wa hivi karibuni dhidi ya Guinea.

Stars ikiwa ugenini, Ivory Coast Jumanne iliyopita ilifanikiwa kupata ushindi muhimu na wa kusisimua wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea ambao walichagua mchezo huo kuuchezea huko kutokana na viwanja vya kwao kutokidhi vigezo vya Shirikisho la soka Afrika, CAF.

Kabla ya mchezo huo, Stars ilikuwa imetoka suluhu na Ethiopia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, matokeo hayo yaliibua maneno maneno mengi kutoka kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa soka.

Matokeo hayo na mchezo uliotajwa kuwa wa kutovutia dhidi ya Waethiopia hao yaliwagawa mashabiki ambapo wapo walioona Stars wana wakati mgumu na pengine hawana matumaini ya kupata tiketi ya kushiriki AFCON ya Morocco.

Lakini pia wapo waliokuwa na matumaini huenda michezo inayofuata Stars ikafanya vizuri na kuendelea kuweka hai matumaini ya kufuzu fainali hizo.

Kimsingi maneno yalikuwa mengi na wapo pia walioanza kulishambulia benchi la ufundi na kusema hawana imani nao katika safari ya kuwapeleka Morocco.

Jambo tunalotaka kusema ni kwamba, hatupaswi kumaliza maneno pale timu yetu inapopata matokeo yasiyotufurahisha , tunapaswa kuendelea kusapoti timu yetu katika kila hali.

Matokeo ya Jumanne iliyopita mbele ya Guinea yametupa majibu hayo, wale waliokuwa wakiibeza na kuikatia tamaa walikosa cha kuongea, lakini wale waliokuwa na matumaini na kuendelea kuiunga mkono ndio waliokuwa na furaha ya kweli.

Timu ya taifa ni timu yetu sote watanzania, sio timu ya mashabiki wa Simba, Yanga wala Pamba, ni timu ya kila Mtanzania bila kujali dini wala kabila lake, tunapaswa kuiunga mkono sote.

Taifa Stars ikipata ushindi ni ushindi wa Watanzania, na hata ikipoteza mchezo ni Tanzania ndio iliyopoteza, tuwe na akiba ya maneno kwa timu yetu.

Nipashe tunawakumbusha mashabiki, kuelekea kukamatia tiketi ya kushiriki Ethiopia na Guinea. Stars bado ina kazi kubwa mbele yake kwa kuwa kuna michezo mingine minne mbele yake katika Kundi H walikopangwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia na Guinea.

Mchezo unaofuata Stars itacheza na vinara wa kundi lao, Congo, ni lazima sasa watanzania tuungane na kuiunga mkono timu yetu kwa kuwatia moyo wachezaji pamoja na kujitokeza kwa wingi uwanjani kila inapocheza kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika michezo minne iliyobaki, Stars ina michezo miwili watakayocheza nyumbani, tujipange kujitokeza kwa wingi kuhakikisha tunakata tiketi ya kushiriki fainali hizo.

Ikumbukwe, baada ya fainali za Morocco, Tanzania kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda tutakuwa wenyeji wa fainali za mwaka 2027, hivyo kushiriki kwetu fainali za 2025 kuna maana kubwa sana.

Hongereni wachezaji Taifa Stars kwa ushindi dhidi ya Guinea, lakini pia mkumbuke watanzania tupo nyuma yenu na tunatarajia makubwa zaidi katika kampeni ya kufuzu fainali hizo za Morocco.