Mashabiki nchini zipeni nguvu Simba, Yanga michuano CAF

Nipashe
Published at 07:47 AM Sep 21 2024
Mashabiki nchini zipeni nguvu   Simba, Yanga michuano CAF
Picha:Mtandao
Mashabiki nchini zipeni nguvu Simba, Yanga michuano CAF

VIGOGO wa kandanda nchini, Simba na Yanga zote kutoka jijiji, Dar es Salaam zinatarajia kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wao wanashuka kwenye uwanja wa Amaan Complex Zanzibar kuwakaribisha CBE kutoka Ethiopia katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 wakati Wekundu wa Msimbazi wao watawakabili Al Ahly Tripoli kutoka Libya kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, mechi ya kwanza wakitoka suluhu.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa walianzia ugenini na wikendi hii watamalizia vibarua hapa nyumbani, Yanga wakicheza leo huko Visiwani Zanzibar na Simba yenyewe itakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa hapo kesho.

Kwa namna mpira wa miguu ulivyo sasa, hakuna timu ambayo unaweza kusema iko katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kutinga hatua ya makundi, wawakilishi hawa wawili wanatakiwa wafahamu bado wana jukumu la kwenda kupambana kusaka ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele katika mashindano hayo ya CAF yanayofanyika kila mwaka.

Simba na Yanga hawatakiwi kuwadharau wapinzani wao kwa sababu yoyote ile, wasiwe na mawazo kwamba wao majina yao ni makubwa au wanajivunia wanacheza kwenye ardhi ya nyumbani kwa Mama Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Mwinyi.

Wachezaji wetu wa Simba na Yanga wanatakiwa kuingia uwanjani wakifahamu wamebeba furaha ya Watanzania na wanatakiwa kuilinda kwa ‘Jasho na Damu’ na si vinginevyo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi na Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davis, wanatakiwa kukamilisha vyema tathmini na kupanga wachezaji ambao wataingia uwanjani kusaka ushindi huku wakitumia mapungufu ya wapinzani ambayo waliyabaini katika michezo ya awali na hatimaye kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Viongozi wa Simba na Yanga, huu ni wakati mwingine muhimu wa kutimiza majukumu yenu kwa kufanya kila kinachotakiwa na kinachowezekana ili kupata ushindi na hatimaye kutinga hatua ya makundi huku Azam FC na Coastal Union ambazo zimetolewa na timu nyingine za Tanzania kuendelea kujifunza namna ya kupambana kimataifa.

Tunahitaji kuona viongozi wanazidisha umoja na ushirikiano bila kuwaweka pembeni ‘wakubwa’ wa soka Tanzania (TFF), katika kuhakikisha ushindi unapatikana na malengo ya kutinga hatua ya makundi kwa mara nyingine yanatimia.

Lakini ili haya yote yatimie, huu ni wakati muhimu kwa mashabiki wote wa soka Tanzania kuungana pamoja katika kutoa sapoti kuwashangilia wachezaji wetu wa Simba na Yanga wanapokuwa dimbani wakipeperusha bendera ya nchi katika mashindano hayo ya kimataifa.

Mashabiki ni sawa na mchezaji wa 12 uwanjani, hawa ni kiungo muhimu katika kufikia malengo ya timu iwe klabu au timu ya taifa, mashabiki wanatakuwa kuwa kitu kimoja kwa sababu kufanya vyema kwa timu zote mbili, kutaipa Tanzania nafasi ya kutoa wawakilishi wanne kwenye michuano hiyo ya CAF.

Umefika wakati ile tabia ya kuwapa ushirikiano wapinzani na kutoa ‘siri’ ili upande wa pili ufungwe, usichukue nafasi kwa maslahi makubwa ya nchi na si jambo lingine lolote.

Tanzania inahitaji kuendelea kupeperusha bendera yake katika mashindano hayo huku tukiwa na kiu ya kuliona taji la Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho Afrika linatua nchini, na ili tufike huku ni lazima tuonyeshe mabadiliko kwa kushangilia wachezaji wetu na kuweka pembeni ushindani wetu uliopo tunapokutana kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

Tunahitaji kuona mechi nyingi za kimataifa zinafanyika hapa nchini, na ili uhondo huu upatikane, huu ni wakati muhimu wa kuwaombea dua njema wawakilishi hawa waliobakia na wanaopaswa kulitekeleza kwa pamoja na wingi wao ni mashabiki watakaokwenda uwanjani.

Mashabiki wanatakiwa kuwapa nguvu wachezaji, kuwashangilia kutasaidia kuwaongezea ari ya kupambana na si kuwazomea au kuwashangilia wageni, tabia hii tuzike rasmi na kufungua ukurasa mpya pale Simba na Yanga zinapokuwa kwenye kibarua cha michuano ya CAF.

Kila la heri Yanga, kila la heri Simba katika mechi za CAF.