Kila kukicha ukatili mama, mtoto tunahitaji staili mpya ukomeshaji

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 01:16 PM Sep 20 2024
Kila kukicha ukatili mama, mtoto  tunahitaji staili mpya ukomeshaji
Picha:Mtandao
Kila kukicha ukatili mama, mtoto tunahitaji staili mpya ukomeshaji

UKATILI dhidi ya wanawake na wasichana ni sehemu ya ukiukwaji wa haki za binadamu, inazochangia kuathiri zaidi ya wanawake milioni 1.3 duniani kote.

 Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake, UN Women, ambayo imewahi kuitoa na kusambazwa katika vyombo vya habari.
 
 Kwa mujibu wa shirika hilo, majanga, mizozo na vita vinazidi kuongeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na kuchochea visababishi na hatari zaidi vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
 
 Hapa nchini, inaelezwa kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika kipindi cha maisha yao.
 
 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, anasema taarifa za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria inaonesha pia kwa mwaka 2015/16 asilimia 20 ya wanawake wa umri huo wameingiliwa kimwili bila ridhaa yao.
 
 Kwa hali kama hiyo, ninadhani kuna haja ya kuwa na mikakati madhubuti ya kudhibiti vitendo vyote vya ukatili ili kuwalinda wanawake na wasichana ambao wanatajwa kuwa waathirika wakubwa.
 
 Wizara inasema kuna Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Tanzania (MTAKUWWA) unaolenga kuongeza msaada wa kielimu ili kuwajengea waathirika uelewa.
 
 Hilo ni jambo jema, kwani mtu akiwa na uelewa wa kutosha kuhusu haki yake, inaweza kuwa rahisi kwake kutoa taarifa anapoona viashiria vya ukatili au anapofanyiwa vitendo vya ukatili.
 
 Katika maeneo mbalimbali, kuna kamati za ulinzi wa wanawake na watoto 1,8126 ngazi ya taifa, mkoa, halmashauri, kata, vijiji na mitaa. Kwa kutumia nyenzo hizo, inaweza kuwa rahisi kudhibiti ukatili.
 
 Serikali ina wajibu wa kuandaa mikakati madhubuti iliyoboreshwa itakayosaidia kuimarisha Kamati za MTAKUWWA ikiwamo kutenga bajeti kwa kushirikiana na wadau, ili kutekeleza mpango kazi huo.
 
 Pia, jamii iwe tayari kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabana wale wote wanaoshiriki vitendo vya ukatili hata kama watuhumiwa watakuwa ni ndugu.
 
 Wapo baadhi ya watu ambao huwaficha watuhumiwa hasa wale wanaobainika kuwa wahusika ni ndugu au kumalizana na wale wanaofanya vitendo hivyo kwa kulipwa fedha.
 
 Ni aibu, mtu anabaka au analawiti, halafu anafichwa eti kwa sababu ni ndugu au anatoa fedha ili kumalizana na wazazi ama familia, kitendo ambacho kinaweza kusababisha ukatili kuendelea ndani ya jamii.
 
 Wataalam wa saikolojia wanasema, ukatili unaweza kuwa ukatili wa kingono, unaoweza kusababisha magonjwa kama UKIMWI, lakini pia kuna ukatili wa vipigo na kwamba suala la athari kisaikolojia zinaweza kufanana.
 
 Mojawapo ya athari zinazotajwa na wataalam hao ni kutojiamini, kutoamini watu, kutojikubali na kwamba mazingira kama hayo, wanatakiwa kukutana na watu wa saikolojia ili kuzungumza nao, kuwashauri ili kuwaweka sawa.
 
 Wanasema ukatili wa kijinsia una madhara mengi, na kwamba matokeo yake ni mabaya kwa wanawake na watoto, kwa kuwa yanaweza kudumu katika kipindi chote cha maisha ya ‘manusura’ kama hawakupata wataalam wa saikolojia kwa ajili ya kuwaweka sawa.
 
 Aidha, wanaweka wazi kuwa, ukatili huo unaweza kuharibu fursa ya mtu kuishi maisha mazuri, yenye afya na mafanikio na yanaweza kuathiri mtu kiafya, kimwili, kisaikolojia na kiroho, kuathiri uwezo wa mwanamke kushiriki katika masuala ya kiuchumi na kufifisha uwezo wake katika kuboresha maisha ya familia.
 
 Kimsingi, ukatili huo haupaswi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa wanawake na wasichana wa Kitanzania kwani kama wanavyosema wataalam wa saikolojia,  una madhara makubwa katika maisha.
 
 Mikakati zaidi ni muhimu kwa ajili ya kukomesha ukatili kwa wanawake na wasichana ili waweze kuishi kwa amani katika nchi yao. Jambo la msingi ni kila mmoja kushiriki katika vita dhidi ya vitendo hivyo.