Watu wanaotumia mitandao vibaya wadhibitiwe

Nipashe
Published at 10:31 AM Sep 13 2024
Watu wanaotumia mitandao vibaya wadhibitiwe
Picha:Mtandao
Watu wanaotumia mitandao vibaya wadhibitiwe

MAPAMBANO dhidi ya uhalifu mitandaoni ni jambo muhimu hasa wakati dunia ikiwa kwenye mabadiliko ya kutumia teknolojia ya mawasiliano.

Kuna mambo mengi yanayotokea katika kipindi hiki huku wahalifu wakitafuta mbinu mbalimbali za kuhakikisha wanakwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Dunia kwenda na mabadiliko ya teknolojia ni kurahisisha kazi na kupunguza muda unaotumika kwa binadamu kuifanya kazi hiyo.

Hata hivyo, kuna watu wanaotumia fursa hiyo kujinufaisha na kuona hawaachwi nyuma kwa jambo lolote lile.

Kuna watu wanaotumia teknolojia hiyo kuandika mambo ya uongo kwa kutumia jina la kampuni fulani ionekane kama ndio iliyofanya jambo hilo.

Ndio maana kuna umuhimu wa kuhakikisha kama jambo hilo ni sahihi kutoka kwenye kampuni husika kabla ya kuanza kuishambulia.

Pia, wapo wanaotumia picha za matukio ya zamani na kuzitengeneza ili mradi kuwachafua watu na kuwaharibia wasifu wao. Teknolojia hii isitumike kuharibu badala yake watu waitumie kujifunza mambo yenye maendeleo kwa faida yao na taifa.

Miaka ya nyuma kabla ya teknolojia ya mawasiliano haijabadilika, kazi nyingi zilikuwa zikifanyika kwa kwenda sehemu husika, lakini sasa hivi mtu anaweza kukaa nyumbani na akamaliza kila kitu kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Siku za nyuma sehemu zenye huduma muhimu kama ulipaji wa bili za umeme, maji na benki, mtu ilibidi aende kwenye ofisi hizo hali iliyokuwa ikisababisha msongamo mkubwa wa watu.

Sasa hivi hata ukiwa nje ya nchi unaweza kufanya miamala na kulipia bili zako kwa wakati.

Kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ilikuwa inachukua muda kumtumia ndugu yake pesa, lakini kwa sasa teknolojia imerahisisha, hakuna usumbufu tena.

Lakini, teknolojia hiyo imeingiliwa na kutumika vibaya kwa baadhi ya wahalifu kwenye sekta ya fedha kwa kuwaibia watumiaji na kuwafanya waogope kuitumia.

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), imeeleza wazi kuwa inaendeleza jitihada za kupambana na kudhibiti uhalifu mitandaoni, ikiwamo huduma za kifedha kutokana na kuongezeka mifumo mipya ya mawasiliano ya teknolojia.

Inapokuja teknolojia mpya ni muhimu ikatumika vizuri ili kunufaisha watu na kuondoa ugumu uliokuwapo mwanzo.

Kwa nchini Tanzania, wafanyabiashara, wajasiriamali wamerahisishiwa kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ambapo kwa sasa wanaweza kutuma pesa nje ya nchi na kuletewa bidhaa wanazotaka badala ya kusafiri hali inayowapunguzia gharama.

Katika matumizi ya teknolojia hii pia kunahitajika uaminifu wa hali ya juu ndio maana hata TCRA ikiwa ni mdhibiti wa matumizi mabaya ya mawasiliano imekuwa ikiingilia kati kila inapoona mambo hayaendi sawa.

Kuna wanaotumia teknolojia hiyo pia kwa malengo mabaya ya kuwachafua watu wengine kwenye mitandao.

Hali hiyo imekuwa ikishamiri kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuharibu hali ya hewa na wengine wanaochafuliwa huathirika kisaikolojia.

Viongozi wa juu wanapokuwa kwenye majukwaa wamekuwa wakikemea tabia hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa kama isipodhibitiwa itarudisha nyuma maendeleo.

Duniani mabadiliko ya kiteknolojia hayawezi kuepukika, hivyo ni muhimu wadhibiti wa uhalifu mitandaoni kuwa makini kudhibiti hali hiyo ili kuepuka matumizi mabaya.