MWAKA jana Rais Samia Suluhu Hassan, akiwahutubia viongozi wa Afrika kwenye jukwaa la kilimo (AGRRF 2023), anawaambia lazima marais wahakikishe Afrika inajitosheleza kwa chakula.
Ni katika kusanyiko linaloangazia umuhimu wa kuwekeza katika kilimo biashara ili kulinusuru bara hili na njaa na wakati mwingine uhaba wa chakula usiokuwa na sababu.
Anasema Afrika inajulikana kuwa ina asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo, yapo mabonde na nyanda za kilimo na ufugaji, vipo vijito na mito mikubwa inayofanikisha umwagiliaji.
Sifa hizo zinathibitisha kuwa Afrika haikustahili kulia njaa wala kuagiza ngano, mahindi au nafaka ya aina yoyote kutoka nje.
Rais Samia anahutubia jukwaa la chakula Septemba mwaka jana ambapo leo umetimia mwaka mmoja wa AGRF 2023, ambao unaamsha hamasa za kuwa na suluhu ya changamoto ya chakula hasa kwa kujitosheleza kwa kila namna.
Tukiangalia Tanzania asilimia 60 ya raia ni vijana ambao ni nguvu kazi ambayo inahitaji kula vizuri na kupata lishe bora ili kufanyakazi ya kuibadili nchi kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye utajiri unaoambatana na kujitosheleza kwa chakula.
Ni wazi kuwa juhudi zinafanyika kuwa na chakula cha kutosha na kama serikali inavyoeleza bungeni, Tanzania inajitosheleza kwa chakula ikiwa na zaidi ya asilimia 130 ya nafaka muhimu hasa mahindi na mchele.
Baadhi ya nafaka hasa mahindi huuzwa ukanda wa kusini mwa Afrika kuanzia Zambia na Malawi zinazokabiliwa na njaa.
Ni jambo jema kwa sababu nchi ina mahindi na mchele, hata hivyo wakati umefika kubadilika na kuachana na ulaji wa kimazoea.
Ni vyema kusahau fikra kuwa chakula ni lazima kupata unga wa mahindi kwa ajili ya ugali au mchele ili kupika wali na ngano kutengeneza vitafunwa kuanzia mkate, chapati hadi maandazi.
Tukumbuke kuwa tatizo la kutegemea nafaka moja kama mahindi kwa ajili ya sembe na dona kunasababisha wakati mgumu kwa wananchi sembe inapopanda bei, hasa pale mahindi yanapopungua nchini.
Hamasa ianze sasa Watanzania waanze kuzoea kuchanganya nafaka na mazao mengine mfano mtama, mhogo, viazi na magimbi kupata unga.
Siyo lazima kula ugali wa sembe muda wote, wakati mihogo inaozea shambani. Uwepo unga wa mchanganyiko huo na zifanyike hamasa kubadili mazoea ya unga wa aina moja pekee.
Pia, si lazima kula chapati au vitafunio vya ngano pekee tubadili fikira tuanze kuzichanganye na unga wa ndizi, viazi, vitamu, mbatata, dengu na muhogo.
Kadhalika maandazi nayo mambo yabadilike kuwe na vitafunwa vya unga wa nafaka mbalimbali kupunguza utegemezi wa unga wa aina moja.
Kutegemea ngano pekee kunasababisha Tanzania na Afrika kulia kila siku kuwa kuna uhaba wa nafaka hiyo inayoagizwa kutoka Ukraine na Urusi.
Licha ya rasilimali au nafaka nyingi zilizopo Watanzania wamebaki kulalamikia kukosa chakula au kushindwa kumudu milo mitatu wakati kila kitu kipo.
Si lazima kula wali unaotokana na mchele hata wa mtama unawezekana, mahindi na ngano pia.
Kutegemea maharage muda wote kunasababisha yafikie kilo moja Shilingi 4,000 hasa mijini, inakuwaje watu wasile mbaazi, kunde, choroko, njugu mawe au dengu?
Kuwa na chakula cha kutosha siyo suala la kutegemea mataifa yaliyoendelea wasomi na wataalamu wa Tanzania wapo wabadilishe silica, mazoea ya ulaji ili kila mmoja ale na apate afya.
Ni vyema pia kila mkoa uwe na tathmini ya kujua watu au kaya zisizo na uwezo wa kumudu chakula na kutafuta ufumbuzi.
Katika mkutano wa AGRRF 2023, Rais Samia anaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 283 wanalala njaa barani Afrika.
Katika idadi hiyo Watanzania wako wangapi? Juhudi zifanyike kuwatambua mijini na vijijini na kupata mbinu za kuwasaidia.
Aidha, kazi hiyo iende pamoja na kuhimiza mabadiliko ya mifumo ya kutumia vyakula vya aina mbalimbali ili kila mtu ale na kuondokana na changamoto ya kukosa chakula inayozungumzwa na wengi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED