Jamii isiwe chanzo kusababisha magonjwa ya akili

Nipashe
Published at 03:09 PM Sep 20 2024
   Jamii isiwe chanzo kusababisha magonjwa afya ya akili
Picha:Mtandao
Jamii isiwe chanzo kusababisha magonjwa afya ya akili

WATAALAMU bingwa na bobezi wa magonjwa, afya ya akili na mfumo wa fahamu, kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, wameeleza namna ubongo wa binadamu unavyofanya kazi na kuhifadhi kumbukumbu.

Baadhi ya watu wanaopoteza kumbukumbu, wanaweza kusababishiwa na magonjwa ya akili kama vile msongo wa mawazo, lakini vilevile kupotea kwa kumbukumbu inaweza kuwa tiba muhimu kwa mwili wa binadamu.

Wanatoa mfano kuwa mtu anaposhuhudia mauaji ya kikatili huwa haitoki kwenye kumbukumbu yake na tiba itakayomfaa ni kupoteza kumbukumbu.

Bingwa Mbobezi wa Afya ya Akili na Mfumo wa Fahamu kutoka hospitali hiyo, Dk. Damas Mlaki, anatoa darasa kwa umma akisema jamii inapaswa kuzingatia elimu kuhusu afya ya akili, kwa manufaa ya ustawi wa jamii kwa ujumla.

Magonjwa yanayohusisha ubongo kutofanya kazi yake ipasavyo ni msongo wa mawazo pia kiharusi na waliojeruhiwa sehemu fulani ya ubongo kutokana na ajali na kukwamisha utendaji kazi ya ubongo ipasavyo.

Kadhalika, wapo ambao hupata athari hasa kupoteza kumbukumbu za masuala mbalimbali ambazo ubongo kwa mfumo wake thabiti, huzihifadhi kwa matumizi ya baadaye.

Msongo wa mawazo, sonona, watu kupitia na kuishi kwenye changamoto za maisha ambazo hazipati ufumbuzi wa mapema, huuathiri ubongo na kuhitaji kupewa matibabu ya dawa ama ushauri.

Mbinu za kujikinga na namna ya kufanya ubongo utunze kumbukumbu, inaelezwa kuwa ni kufanya mazoezi ya kimwili na kiakili, lishe bora na kupata usingizi wa kutosha usiopungua saa nane.

Inashauriwa watu kuzingatia usingizi ili kurejesha kumbukumbu na wanafunzi wanapewa angalizo la kutoa muda wa kujisomea kwa kuupumzisha ubongo kwa kupata usingizi jambo ambalo ni muhimu.

“Wanaokesha, wanafunzi kusoma bila kuupa nafasi usingizi ni tatizo. Wanaweza hata wanachokisoma wasikikumbuke katika chumba cha mtihani. Inahitaji ulale angalau saa nane kwa siku, ili kuzihuisha kumbukumbu.”

Mbinu nyingine na kutunza kumbukumbu ni kuupa ubongo mazoezi ya kiakili, wataalamu wanasisitiza pia kuangalia filamu, kusoma vitabu, gazeti, kucheza michezo ya asili kama bao, kwa sababu mtu anatumia fikra ili kumshinda mwenziwe.

Witou kwa watu wote ni jamii izingatie ushauri wa wataalamu wa afya, ili kuboresha ustawi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Vilevile, jamii iache unyanyapaa kwa ambao uwezo wao wa ubongo na kutunza kumbukumbu ni duni hasa watoto, ambao wanapokuwa masomoni hushindwa kufikia wastani wa juu, kwa matamanio ya wazazi au walezi.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Paul Lawala, anasema jamii hasa familia, iache kufananisha uwezo wa ubongo baina ya mtoto mmoja na nduguze, kwani ni kawaida kutofautiana kutokana na ubongo ulivyoendelezwa.

Utafiti unaofanywa maeneo tofauti duniani unaonesha kuwa, uwezo wa ubongo kati ya binadamu mmoja na mwingine hutofautiana, licha ya kuwa pengine wana rika sawa hata kama watoto wa familia moja.

Jamii inatakiwa kuacha kumsema vibaya mtoto mwenye uwezo mdogo hata kumnyanyapaa na ni vyema ubongo wa watoto hao ukaanza kuendelezwa mapema ili kukuza nafasi ya kutunza kumbukumbu za wanachojifunza hata kukuza vipaji vyao.