Ni wakati mwafaka kwa serikali kusikia kilio kuundwa tume huru

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 10:45 AM Sep 18 2024
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani (mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk.
Picha:Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani (mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk.

KWA miezi kadhaa kumekuwapo na taarifa za kutekwa kwa watu na wengine kukutwa wameuawa huku miili yao ikiwa na majeraha kuonesha kwamba kabla ya kufikwa na mauti, walipigwa na kuteswa na watekaji hao.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa kikilalamika mara kwa mara kwamba kimeathirika kwa kiasi kikubwa na matukio hayo kwa madai kuwa baadhi ya wanachama na viongozi wake wametekwa na hawajulikani waliko.  

Pamoja na kulalamika huko, chama hicho kimekuwa kikiomba viongozi na wanachama hao waliotekwa wapatikane ama wakiwa hai au wamekufa. Sambamba na hilo kimekuwa kikilituhumu Jeshi la Polisi kuwa ndilo linalohusika kwa matukio hayo, huku lenyewe likisema hizo ni propaganda na chama kinaficha ukweli. 

Hali hiyo ya utekaji ambayo pia imekuwa ikihusisha watu mbalimbali, ilipata uzito zaidi baada ya kuwapo kwa taarifa za kutekwa na watu waliodaiwa kuwa na silaha kwa aliyekuwa kada na Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA, Ali Kibao. Kada huyo alitekwa Dar es Salaam akiwa kwenye basi akienda Tanga na mwili wake kukutwa eneo la Ununio ukiwa umeharibiwa vibaya kiasi cha kushindwa kutambulika. 

Kutokana na kifo hicho na kukithiri kwa matukio ya utekaji na mauaji ya watu, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maagizo kwamba uchunguzi wa kina ufanyike na apatiwe taarifa. Kauli hiyo iliungwa mkono na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu Mkuu wake, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye alisema uchunguzi ufanyike kama ilivyoagizwa. 

Wakati maagizo hayo yakitolewa na kuungwa mkono, kumejitokeza hoja kinzani kwamba Jeshi la Polisi wala vyombo vya ulinzi na usalama visifanye kazi hiyo kwa sababu baadhi vinatuhumiwa kushiriki matendo hayo ambayo yanatoa taswira hasi kwa Tanzania ambayo imejipambanua kwamba ni kisiwa cha amani na watu wake wanaishi kwa umoja na mshikamano. CHADEMA na makundi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wameshauri iundwe tume huru au tume ya kijaji kuchunguza suala hilo. 

Juzi, wakati wa sherehe za Maulid zilizofanyika kitaifa mkoani Geita, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilihanikiza jambo hilo kwamba ni vyema ikaundwa tume huru kuchunguza matukio hayo ya utekaji na mauaji ambayo yamekuwa yakifanyika katika maeneo mbalimbali nchini. 

Wazo la kuundwa kwa tume huru au ya kijaji ni mwafaka katika mazingira yaliyopo ili kuwapo kwa imani ya watu wote. Kama wahenga wasemavyo mganga hajigangi au kinyozi hajinyoi, ndivyo ilivyo kwa mazingira ya polisi kuchunguza jambo wakati wanatuhumiwa kuwa sehemu ya wahusika. Kwa ujumla, hakutakuwa na imani thabiti kama polisi watashiriki kuchunguza jambo hilo kwa sababu ni watuhumiwa. 

Si mara ya kwanza kuundwa kwa tume huru au za kijaji kwa ajili ya kuchunguza jambo fulani lililojitokeza katika  kwa kuwa  ni utaratibu wa kawaida ili kuwafanya wananchi kuwa na imani na matokeo ya uchunguzi husika. 

Waliomteka Kibao wanadaiwa kuwa askari waliokuwa na silaha na pia waliodaiwa kuwateka viongozi na wanachama wa CHADEMA walijitambulisha kuwa askari polisi, iweje sasa polisi hao hao ndio wahusike na uchunguzi? Tangu lini kesi ya nyani hakimu akawa nyani? Ni dhahiri kwamba kwa hali hiyo haki katu haiwezi kutendeka.   

Kama viongozi wa vyama vya upinzani na BAKWATA walivyoshauri, ni vyema tume huru au ya kijaji hiyo ikaundwa ili ukweli ujulikane badala ya kufanyiwa na vyombo ambavyo vinadaiwa kuhusika na matukio yanayolalamikiwa. 

Ni dhahiri kwamba kilio cha watu mbalimbali kimesikika na serikali ambayo imekuwa ikisema kuwa ni sikivu itakuwa imelipokea wazo hilo, kama  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alivyosema kuwa wanalifanyika kazi, ni imani kwamba jambo hilo litatekelezwa na hatimaye haki kutendeka.