Udanganyifu mitihani unavyokuwa mazoea

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:03 PM Jul 16 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda.

WATAHINIWA 24 wa mtihani wa taifa wa kidato cha sita, wamefutiwa matokeo kutokana na kile kinachoelezwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kuwa ni kufanya udanganyifu kwenye mtihani huo.

Baraza hilo linawataja watahiniwa waliofutiwa matokeo ya mtihani huo kuwa ni wale waliobainika kuingia na simu katika vyumba vya mtihani, huku wengine wakiwa na notisi na wengine wakisaidiana kufanya mitihani.
 
 Idadi hiyo ya waliofutiwa matokeo ya mtihani huo, imekuwa kubwa zaidi kuliko ya mwaka jana, kwani mwaka huo baraza lilitangaza kufuta matokeo ya watahiniwa 11, sababu ikiwa kufanya udanganyifu.
 
 Katika matokeo ya mtihani huo wa kidato cha sita kwa mwaka 2022, watahiniwa 15 walifutiwa matokeo bado sababu kuu ikiwa ni ya udanganyifu ambao inaonekana haujapatiwa suluhisho la kudumu.
 
 Nimejaribu kukumbishia miaka michache ya nyuma, lakini inaonekana kila mwaka ambao baraza hilo limekuwa likitangaza matokeo, huwa kuna watahiniwa wanaofutiwa matokeo kutoka na sababu hizo.
 
 Mtindo huo utaendelea hadi lini? Lengo lake ni nini? Kwa nini mwanafunzi akubali kufaulu kwa udanganyifu badala ya kutumia elimu aliofundishwa darasani? Mwisho wa udanganyifu ni nini?
 
 Udanganyifu katika mitihani ni janga ambalo linaangamiza elimu ya Tanzania kimya kimya likiwa limejificha, hivyo tukiridhibiti, tutakuwa tumeokoa elimu inayotishiwa na vitendo hivyo.
 
 Mtindo au tabia hiyo ya wizi na udanganyifu wa mitihani, vimekuwa vikiporomosha elimu, kutokana na ukweli kwamba, wanafaunzi wanaofaulu kwa njia hiyo, hawawezi kufika mbali kielimu.
 
 Kama ni kukemea wizi huo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilishakemea sana, ninadhani kilichobaki ni kuchukua hatua ambazo zitawafanya wahusika waogope kufanya udanganyifu.
 
 Wizara isiishie kukemea kwa kutumia vyombo vya habari, badala yake ichukua hatua kali kwa wahusika, ili kuwa fundisho kwa wahusika na hata kwa wengine wanaojipanga kufanya udanganyifu.
 
 Udanganyifu ukifanyika, uchunguzi ukawabaini wahusika, ni vyema wasiishie kufutiwa kisha wakapangiwa siku nyingine ya kufanya mtihani, badala waadhibiwe kulingana na makosa yao.
 
 Vinginevyo vitendo vya udanganyifu vitaendelea kuripotiwa kila matokeo yanaotangazwa kana kwamba imeshindikana kuwadhubiti wanaoshiriki mchezo huo mchafu unaporomosha elimu.
 
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema, wizara imebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu hushiriki vitendo hivyo, na kwamba vitendo hivyo ni sawa na  uhujumu uchumi.
 
 Sasa kama ni sawa na uhujumu uchumi, basi ni vyema wahusika wanaobaibika kukutwa na hatia, wahukumie kulingana na jinsi adhabu za uhujumu uchumi zilivyo, ili kukomesha udanganyifu.
 
 Si sahihi kuendelea kufumbua macho wahujumu uchumi, badala yake wachukuliwe hatua stahiki, ili kulinda elimu isiendelee kuporomoka kutokana na tamaa ya watu wachache.
 
 Ikumbukwe kuwa, matatizo katika ubora wa huduma nchini, yanagusa sekta zote, ikiwamo elimu, hivyo, wakati serikali ikiwa na wajibu wa kupanga, kutekeleza na kusimamia utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo, ni muhimu kukumbushana umuhimu wa elimu katika kuchochea maendeleo ya sekta nyingine.
 
 Vilevile udanganyifu katika mitihani una madhara mengi, ikiwamo kuzalisha wataalamu wasiokuwa na viwango, kutokana na wamewezesha bila kuwa na sifa za kustahili kuendelea na masomo.
 
 Hivyo, NECTA na serikali kwa ujumla ni muhimu kuongeza au kubuni  mikakati zaidi ya kupambana na watu ambao wanafanya udanganyifu kwenye mitihani, ikiwamo kuwabaini wasimamizi na walimu anbao hushirikiana kwa namna moja au nyingine kufanya udanganyifu huo.